BAADA ya kifo cha mshambuliaji wa Nigeria, Abubakar Lawal anayeichezea Klabu ya Vipers ya Uganda, Mtanzania Naima Omary anahusishwa na tukio hilo, lililotokea asubuhi ya Jumatatu ya Februari 24, mwaka huu na kuzua sintofahamu kubwa.
Kifo cha mshambuliaji huyo kimeibua utata na sintofahamu kutokana na taarifa tofauti ambazo zimekuwa zikitolewa juu ya chanzo chake.
Moja ya ripoti, zimedai kuwa mchezaji huyo amefariki kutokana na ajali ya gari, huku taarifa ya awali iliyotolewa na Polisi Uganda imeonyesha chanzo tofauti na ajali iliyoeleza alijirusha ghorofani muda mfupi baada ya kukutana na rafiki yake wa kike ambaye ni Mtanzania.
“Kitengo cha Polisi cha Kajansi kinachunguza mazingira ya kifo cha kusikitisha cha raia wa Nigeria, Abubakar Lawal, mchezaji wa kandanda katika klabu ya Vipers, anayedaiwa kuanguka kutoka ghorofa ya tatu ya Voicemall Shopping Arcade asubuhi ya Februari 24, 2025.
“Taarifa za awali zinaeleza kuwa, Lawal alifika katika jumba hilo la maduka akiwa na gari lake lenye namba za usajili UBQ 695G kukutana na Naima Omary, anayeishi chumba namba 416 tangu Februari 20, 2025,” inafafanua taarifa hiyo.
Baada ya taarifa hiyo, Jeshi la Polisi Uganda linamshikilia Naima Omary, kwani ndiye mtu wa mwisho kukutana na mchezaji huyo kabla ya kifo chake.
Naima yupo Uganda kwa ufadhili maalum (Scholarship) ili kuendeleza kipaji chake cha kucheza Mpira wa Kikapu ‘Basketball’ katika Chuo cha St Mary’s.
Mwanzoni ilielezwa nyota huyo mwenye miaka 29, alikuwa akielekea kwenye uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo wa St. Mary’s uliopo mjini Entebbe, Mkoa wa Kati Uganda, lakini alipata ajali katika barabara ya Entebbe iliyokatisha uhai wake.
Mkuu wa Mawasiliano wa Vipers, Abdul Wasike, alithibitisha kuhusu habari hiyo ya kusikitisha siku ya Jumatatu. “Ni siku ya huzuni wakati tunapotoa taarifa kuhusu kifo cha mchezaji wetu Lawal. Bado tunakusanya taarifa zaidi kuhusu ajali hiyo,” alisema Wasike.
Katika taarifa ya Polisi ilieleza Naima Omary anayehusishwa na nyota na nahodha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta, alikuwa akiishi katika jumba hilo sambamba na mshambuliaji huyo kabla ya ajali hiyo iliyotokea kuacha maswali.
Mshambuliaji huyo aliyekuwa na mchango mkubwa katika klabu ya Vipers, alijiunga nayo mwaka 2022, akitokea AS Kigali ya Rwanda, huku akiwahi kuchezea pia timu mbalimbali zikiwemo za Kano Pillars FC, Wikki Tourists FC na FC Nasarawa za kwao Nigeria.
Ibada ya kumuombea nyota huyo inafanyika leo Alhamisi kwenye Uwanja wa St. Mary’s, Kitende, kisha kusafirishwa kwa ajili ya maziko kwao Nigeria.