Rekodi yamtesa Fadlu Simba | Mwanaspoti

Kocha wa Simba Fadlu Davids amesema mechi mbili zijazo zinaweza kutoa picha halisi ya ubingwa kwa timu yake msimu huu.

Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 na Azam FC juzi na kuanza kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa huo msimu huu kwa kuwa ikishinda kiporo chake itakuwa nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi moja.

Akizungumza na Mwanaspoti Fadlu amesema michezo miwili ijayo ndiyo ile ambayo iliwatibulia mzunguko wa kwanza, wataanza kwa kuvaana na Coastal Union ambao walitoka nao sare ya mabao 2-2, lakini pia watavaana na Yanga ambao walipoteza kwa bao 1-0 zikiwa ndiyo pointi pekee ambazo walidondosha kwenye ligi kabla ya mchezo wa Azam.

Simba ambayo inashika nafasi ya pili katika ligi imecheza mechi 20 mpaka sasa, huku ikibeba jumla ya alama 51 na kufunga mabao 40.

Fadku amesema kama watapoteza mechi hizo basi timu yake itakuwa imejiweka kwenye hatari kubwa ya kupoteza ubingwa, kwani itakuwa imepoteza pointi nyingi na itakuwa ngumu kumfikia aliyeko kileleni.

“Mechi kubwa zilizopo mbele yetu ni hizi za sasa dhidi ya Yanga na Coastal, hizi zingine tumeshamalizana nazo, lakini napata wakati mgumu kutokana na rekodi za mzunguko wa kwanza.

“Kwa sasa akili zipo katika mbio za ubingwa kwani bado ziko wazi na mwanga unaonekana ila tukifanya makosa mechi mbili zijazo nuru itazima kabisa.

“Hizi kwetu ni mechi zinazobeba ajenda ya ubingwa na hatutacheka nazo kabisa, kwani tunahitaji alama sita za nguvu zitakazotuweka katika nafasi nzuri.”

Coastal Union inashika nafasi ya nane katika msimamo ikiwa na jumla ya alama 24, hivyo itataka kupambana kuhakikisha inapata ushindi kwenye mchezo huo utakaopigwa wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Related Posts