Dodoma. Serikali inatarajia kujenga shule 103 za sekondari za elimu ya amali nchini ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi watakaomaliza darasa la saba na la sita watakaomaliza kwa pamoja mwaka 2028.
Mkurugenzi wa Elimu Msingi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Abdul Maulid ameyasema hayo leo Jumatano Februari 26,2025 wakati wa mkutano wa pamoja wa tathimini ya maendeleo ya sekta ya elimu.
Akielezea utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 na mitalaa mipya, amesema Serikali itajenga shule hizo na mwaka huu wanaendelea kukamilisha shule 26 za amali ambazo ziko katika mikoa mbalimbali.
“Kwa hiyo shule zinazojengwa zitakuwa pamoja na vifaa vyake. Vyuo vyetu vyote vitatoa walimu kwa ajili ya shule za msingi, zamani vilikuwa vinatoa walimu kwa ajili ya shule za msingi na sekondari,” amesema na kuongeza:
“Serikali tunajiandaa itakapofika mwaka 2027 kuna watakaokuwa wanamaliza darasa la sita na la saba, wote watahitaji kwenda sekondari tumejiandaa kwa ujenzi wa shule na ajira za walimu.’’
Amesema wana mpango mkakati wa kuzalisha walimu wa amali ambapo Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo cha Mtwara na Chuo cha Mtwara Ufundi sasa vitakuwa ndani ya MUST kwa ajili ya kutoa walimu wa elimu ya amali.
Maulid amesema kwa sasa wataalamu kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTIVET), wamebaini kuwapo kwa shule 99 zinazokidhi vigezo vya kuto elimu ya amali.
Hata hivyo, amesema shule 39, zikiwamo 25 za Serikali ndizo walizoona kuwa zinafaa kuanza kutoa mafunzo hayo.
Amesema katika awamu hiyo ya kwanza wanafunzi 2,000 kati yao 184 wenye mahitaji maalumu, waliingia katika mikondo mbalimbali ya elimu ya amali.
Maulid amesema kuwa kulikuwa na upungufu wa walimu wa amali 4633, lakini Serikali imetoa kibali kwa ajili ya kuwaajiri walimu hao.
Aidha, amesema walitakiwa kuanza elimu ya amali kwa kidato cha tano mwaka jana, lakini hawakuweza kutokana na kutofanyika kwa mafunzo ya walimu na ukosefu wa vitabu.
Hata hivyo, amesema mwaka huu wanatarajia kuanza masomo hayo kwa kidato cha tano.
Kuhusu changamoto, Maulid amesema changamoto waliyokutana nayo ni wingi wa wanafunzi.
Amesema katika kuitatua walijenga madarasa 79,000 na vyoo 160,000 ili kupunguza idadi ya wanafunzi katika madarasa yaliyokuwa na msongamano wa wanafunzi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Martha Makula ameshauri bajeti ya elimu iongezwe na kufikia asilimia 20 ya bajeti ya kila mwaka na kutoa msamaha wa kodi kwa vifaa vya elimu vinavyoingizwa hapa nchini.
Akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amesema, kauli mbiu katika mkutano huo ni mageuzi katika sekta ya elimu kwa maendeleo endelevu.