Siri imefichuka… Hapa ndiyo jeuri ya Yanga ilipo

KUNA kitu Yanga inakifanya kwa sasa, ikipambana kuhakikisha kwamba inaikamata rekodi ya Simba ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo katika miaka ya karibuni, kabla haujahamia Jangwani kwa misimu mitatu iliyopita.

Kazi kubwa inafanyika katika kipindi ambacho benchi la ufundi la timu hiyo likiwa chini ya kocha mpya, Hamdi Miloud, lakini haijaleta shida kwa wasaidizi aliokutana nao katika kikosi hicho cha mabingwa mara 30 wa Ligi Kuu.

Lakini, kocha Miloud amekiangalia kikosi chake kwa umakini mkubwa, kisha akasema anaamini kwa aina ya viungo alionao kwa sasa wapinzani watakuwa na wakati mgumu kwenye kila mchezo.

Yanga kwa sasa inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 55 baada ya kucheza michezo 21, ikifunga mabao 55 na kuruhusu tisa.

Yanga ndiyo timu yenye namba nzuri zaidi Ligi Kuu hadi sasa. Imefunga mabao sawa na pointi ilizokusanya kwenye michezo 21, lakini wachezaji wake wanaongoza kwa mabao, pamoja na pasi za mwisho.

Kwenye michezo hiyo imepoteza miwili dhidi ya Azam na Tabora United na sare mmoja dhidi ya JKT Tanzania.

Akizungumza na Mwanaspoti, Miloud amesema kama kuna idara inayoipa Yanga jeuri kubwa basi ni eneo la kiungo na kikosi chake kimebarikiwa kuwa na wachezaji wanaojua kutengeneza nafasi na kukaba.

Kocha huyo amesema viungo hao wamekuwa wakitengeneza ugumu mkubwa kwa wapinzani, kutokana na ubora wao na licha ya kujua kutengeneza nafasi pia wanaweza kufunga.

“Unapokuwa na viungo kama Aziz ( KI Stephane), Maxi (Nzengeli), Pacome (Zouzoua), Duke (Abuya), Chama (Clatous) na wengine unaona namna unavyopata nafasi kubwa ya kuwa na watu bora ambao wakati wowote wanaweza kubadilisha kasi ya timu,” amesema Miloud.

“Ukiwa na timu ya namna hii ya watu bora ambao wanashindana vizuri eneo la mazoezi, kocha unapata wakati mgumu kuchagua nani acheze kwa kuanza na nani asubiri nadhani pia wapinzani wetu wanapata shida kuizuia Yanga eneo hili.”

Kocha huyo amesema licha ya kuwa na viungo bora watengenezaji, pia timu hiyo ni tofauti na vikosi vingine kwani imebarikiwa kuwa na viungo wakabaji wenye uwezo wa hali ya juu uwanjani jambo ambalo limeifanya timu hiyo hadi sasa kuruhusu mabao machache.

“Angalia nyuma yao kuna Aucho (Khalid), Sure Boy (Salum Abubakar), Mudathir (Yahya),unaweza kuona namna mnaweza kuwa na nguvu mbele ya mabeki wa kati bado kuna viungo wengine kama Jonas (Mkude), Farid (Mussa), Shekhan (Khamis) na Aziz (Adambwile) hawajapata nafasi sana ya kucheza lakini unaona ubora wao,” amesema kocha huyo.

Miloud ameongeza kuwa, uwepo wa viungo hao bora unawapa nafasi rahisi washambuliaji wa timu hiyo kuendelea kufanya vizuri kwenye mechi zao kwa kuwa soka wanalocheza pamoja na ubora wa eneo la kiungo linaipa timu yake nafasi ya kufanya vizuri kwenye kutengeneza nafasi, huku pia washambuliaji wake Prince Dube na Clement Mzize wakiwika kwenye ufungaji.

Related Posts