Watoto wawili kati ya 100 huzaliwa na tatizo la moyo nchini

Dodoma. Watoto wawili kati ya 100 huzaliwa na tatizo la moyo nchini kila mwaka, huku wataalamu wakibainisha kuwa wengi hawagunduliki mapema na hufariki wakitibiwa magonjwa mengine ikiwemo kukosa pumzi, kifua kikuu na nimonia.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kupitia wataalamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI kupitia huduma mkoba katika mikoa 20, walibaini pia asilimia sita hadi tisa ya watu wazima hugundulika kuwa na ugonjwa huo.

Akitaja takwimu hizo wakati wa hotuba maalum kuhusu mafanikio ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kipindi cha miaka minne leo Februari 26, 2025, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dk Peter Kisenge amesema tatizo ni kubwa na halipaswi kufumbiwa macho.

Dk Kisenge amesema wastani huo ni kutokana na utafiti wanaoufanya kupitia wataalamu wao ikiwemo tiba mkoba, iliyofanyika katika mikoa 20 ya Tanzania ambako walikutana na Watanzania wengi waliokuwa na matatizo hayo.

Amesema yapo mambo mengi yanayoweza kusababisha matatizo hayo, hasa kwa watu wazima ambayo ni pamoja na mlo usiokuwa na mpangilio mzuri hasa kwa mama wajawazito, kutofanya mazoezi, uzito uliopitiliza lakini kutofanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

Hata hivyo, mtaalamu wa magonjwa ya wanawake na watoto Dk Thomas Jakob ametaja sababu kuu inayosababisha watoto wengi kuzaliwa na matatizo ya moyo, ni kwa mama mjamzito ambaye anachelewa kujifungua.

Dk Thomas amesema mwanamke anatakiwa kutumia muda mfupi mara anapopata uchungu wa uzazi kuwa ameshajifungua, lakini akichelewa husababisha mapigo ya moyo ya mtoto kwenda haraka na mwisho hutengeneza tundu la moyo.

“Tatizo la kuchelewa kujifungua ni moja ya vitu vinavyosababisha watoto wengi kupata shida ya kuwa na matundu kwenye moyo, hili linatokana na mwanamke kutohudhuria kliniki kwa muda na vipindi vinavyotakiwa,” anasema Dk Thomas.

Kwa upande wake, Savela John (28) ambaye anaishi na mtoto wa miaka miwili mwenye tatizo la moyo, anasema hakuwa na ufahamu iwapo kuchelewa kujifungua husababisha tatizo hilo.

“Huyu ni mtoto wangu wa pili, alizaliwa vizuri lakini baadae akawa haongezeki uzito kwa kiwango kinachotakiwa, tulimpima magonjwa yote ikiwemo mimi na mzazi mwenzangu lakini hatukuwa na shida ndipo mwaka huu ikagundulika mwanangu ana shida katika moyo wake na tumeshauriwa twende Dar es Salaam kwa utaalamu zaidi,” anasema Savela.

Kuhusu nini kifanyike Dk Thomas amesema, “Mwanamke akihudhuria kliniki kwa wakati na kila mara awe anafanyiwa uchunguzi kuhusu mtoto aliye tumboni pamoja na kupewa dawa na vyakula vinavyompasa, hilo tatizo linaweza kuepukika.”

Takwimu zinaonyesha zaidi ya watoto 13,800 huzaliwa na changamoto za moyo kila mwaka nchini.

Hata hivyo, asilimia 70 ya gharama za matibabu kwa watoto huchangiwa na serikali, hata hivyo bado asilimia 80 hawamudu gharama hizo kwa asilimia 30 iliyobaki, ambapo kiwango cha gharama za upasuaji kwa mtoto mmoja ni kati ya Sh4 milioni hadi Sh15 milioni.

Takwimu za JKCI zinaonesha taasisi hiyo hufanya upasuaji kwa watoto 357 kila mwaka na kwamba kati ya 13,800 wanaozaliwa na matatizo ya moyo 4,000 watahitaji upasuaji.

Kwa mujibu wa JKCI watoto walio wengi huzaliwa na hitilafu katika moyo na kinachosumbua ni tundu kwenye moyo.

Wengi wao vyumba vya juu vya moyo huwa na uwazi na wakati mwingine husababishwa na kutojitengeneza vizuri kwa mishipa ya moyo au vyumba vinne vya moyo.

“Kwa kawaida mtoto anatakiwa kuzaliwa na vyumba vine vya moyo, lakini wengi huzaliwa na vyumba viwili pekee na viwili havipo au havijajitengeneza vizuri yaani muunganiko hauko vizuri na mwingine mishipa haikukua kabisa,” amesema Dk Kisenge.

Amesema asilimia 90 ya magonjwa ya moyo kwa watoto yanatibika na asilimia 10 hushindikana.

Amesema bado ugunduzi wa watoto wenye matatizo ya moyo ni hafifu kwani wengi hufariki kwa nimonia au kifo cha ghafla na wengine wanatibu kifua kikuu kumbe ni ugonjwa wa moyo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto JKCI Surender Kuboja amesema magonjwa ya moyo yanachangia kwa kiasi kikubwa katika vifo vya watu duniani huku yakishambulia watoto, watu wa umri wa kati pamoja na wazee.

“Kwa watoto tatizo hili linatokana na kurithi, kuzaliwa nalo au Rheumatic fever, (homa ya riumatiki), kwa upande wa kuzaliwa takribani watoto 1000 kati yao wanane mpaka 10 hufariki kutokana na magonjwa ya moyo na ile ya rheumatic fever kati ya watoto 1000, 10 mpaka 20 wanaugua ugonjwa huo,” amesema Dk Kuboja.

Akizungumzia mafanikio katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa awamu ya sita, Dk Kisenge amesema Taasisi hiyo imewafikia jumla ya wagonjwa 745,837 ambapo kati yao, watu wazima walikuwa 674,653 na watoto walikuwa 71,184 huku watu 30,645 ndiyo waliolazwa.

“Wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) upanga walikuwa 513,484 kati ya hao watu wazima walikuwa 470,119 na watoto walikuwa ni 43,365 lakini waliolazwa walikuwa 17,668,” amesema Dk Kisenge.

Ametaja mafanikio mengine ni kuongezeka kwa matawi ya Hospitali hiyo ikiwemo Dar Group iliyopo eneo la TAZARA na kwa sasa wameelekea Arusha ambako nako watakuwa na tawi kabla ya kufikia kanda zote.

Katika maelezo yake, Wataalamu wa JKCI walivuka mipaka ya nchi na kwenda kutoa huduma za matibabu ya moyo katika nchi za Malawi, Zambia na Jamhuri ya Watu wa Comoro ambako walitibu jumla ya wagonjwa 1,189 na wagonjwa 262 walipatiwa rufaa ya kuja Tanzania.

Related Posts