WAZIRI KOMBO AWASILI MALAWI KUHUDHURIA MKUTANO WA SITA WA JPCC.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amewasili jijini Lilongwe, Malawi, kushiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi.


Mkutano huo wa ngazi ya mawaziri utafanyika tarehe 26 Februari 2025, ukiwa ni jukwaa muhimu la kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kiuchumi kati ya Tanzania na Malawi.

 
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu Banda jijini Lilongwe Mhe. Kombo amepokewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Patricia Nangozo Kainga (Mb), na Balozi wa Tanzania Malawi, Mhe. Agnes Kayola.

Mkutano wa Sita wa JPCC utajadili masuala muhimu ya kuendelea kuimarisha Ushirikiano kupitia sekta za biashara, uwekezaji, miundombinu, elimu, afya, ulinzi na usalama, pamoja na fursa zinazopatikana kwenye maeneo ya ushirikiano katika sekta za kipaumbele.

Mkutano huo pia, utafanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kutatua changamoto mbalimbali.

Viongozi wa pande zote mbili wanatarajiwa kusaini makubaliano mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya Mataifa yote mawili.



Related Posts