Zanzibar ina mtaalamu mmoja wa upasuaji moyo

Unguja.  Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa wataalamu wa magonjwa ya moyo, ambapo kwa sasa kuna wataalamu wa moyo wanne pekee, huku mmoja tu akiwa na uwezo wa kufanya upasuaji wa moyo.

Hali hii imebainika wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Moyo Tanzania (CardioTan 2025) pamoja na mafunzo ya awali ya uokoaji wa maisha katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta ya utalii.

Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Wizara ya Afya.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Februari 24, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Amour Suleiman Muhamed, amesema hali si nzuri katika sekta hiyo, kwani vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo vinachangiwa kwa kiasi kikubwa na uhaba wa wataalamu.

Dk Amour ameeleza kuwa kuna haja ya kuwajengea uwezo wataalamu wengi zaidi, ili kuhakikisha huduma za matibabu ya moyo zinapatikana kwa uhakika kisiwani humo.

“Kwa sasa, Zanzibar ina jumla ya wataalamu wanne wa moyo, lakini ni mmoja tu anayeweza kufanya upasuaji wa moyo. Hii inaonyesha kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuhakikisha tunawahamasisha watu wengi kusomea fani hii ili waweze kuokoa maisha,” amesema Dk Amour.

Aidha, amefafanua kuwa kwa upande wa madaktari bingwa wa huduma za dharura, Zanzibar ina madaktari watatu waliopo kazini, huku wengine watano wakiwa bado masomoni.

“Kwa idadi ya watu wa Zanzibar, hii ni idadi ndogo sana. Njia pekee ya kupunguza pengo hili ni kushiriki kikamilifu katika mafunzo kama haya ili kuongeza idadi ya wataalamu kwa muda mfupi na kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo,” ameongeza.

Dk Amour pia amesisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo wahudumu wa afya katika ngazi ya jamii, kwani wao ndio wa kwanza kukutana na wagonjwa kabla ya kufikishwa kwa madaktari bingwa. Hii itawawezesha kutoa msaada wa haraka na muhimu kwa wagonjwa wa moyo kabla ya kupokewa hospitalini.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Tatizo Waane, amesema taasisi hiyo imejidhatiti katika kukuza huduma za uchunguzi, matibabu na utafiti wa magonjwa ya moyo nchini.

“JKCI ina wataalamu wengi wa magonjwa ya moyo, pamoja na wale wanaofanya uchunguzi na upasuaji bila kufungu kifua. Pia, tunao wataalamu wanaofanya kazi ya kuzuia matatizo ya moyo na tunatoa huduma kwa wagonjwa kutoka nchi jirani na hata wale wanaokuja kwa ajili ya ‘utalii tiba’,” alisema Dk Waane.

Akizungumzia mkutano huo, amesema unalenga kuandaa mkutano mkuu wa masuala ya moyo utakaofanyika Aprili 10 hadi 12, 2025, Zanzibar utakaowakutanisha wataalamu wa moyo kutoka mataifa mbalimbali.

Hii itakuwa mara ya pili kwa mkutano wa aina hii kufanyika Zanzibar, baada ya ule wa mwaka jana ulioshirikisha wataalamu kutoka zaidi ya nchi 40. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo.

Katika mkutano huo, wataalamu watapata fursa ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu magonjwa ya moyo, uchunguzi, matibabu na changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma za moyo, ikiwa ni pamoja na njia bora za kufanya vipimo vya moyo.

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Ahmed Nassor Mazrui amesema JKCI imekuwa mshirika wa karibu wa Wizara ya Afya Zanzibar katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo na mishipa ya damu kwa wananchi.

“Leo hii, kwa kushirikiana na Shirika la Bima Zanzibar, wameanzisha programu ya utoaji wa huduma za dharura na uokoaji. Programu hii inalenga mashirika ya umma na binafsi, kampuni na hoteli,” amesema Waziri Mazrui.

Alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wahudumu wa afya, wafanyakazi wa hoteli, pamoja na watoa huduma za jamii na utalii wanajengewa uwezo wa kutoa msaada wa haraka na sahihi ili kuokoa maisha ya watalii, wageni na jamii kwa ujumla.

Pia amesisitiza kuwa uwepo wa miundombinu bora ya huduma za dharura utasaidia kukuza uchumi wa Zanzibar kwa kuvutia idadi kubwa ya watalii nchini.

Related Posts