Amiry Matumla Atamba Kumchapa Mnamibia

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

MCHEZAJI wa ngumi za kulipa nchini Amiri Matumla ambaye ni mtoto wa Bondia Mstaafu; Rashidi Matumla amejitapa kumchapa mpinzani wake Pauls Amavila raia wa Namibia katika pambano litakalopigwa leo Februari 28,2025 katika ukumbi wa Soko la Magomeni Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana wakati wa utambulisho wa mabondia watakaozichapa katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Kampuni ya Mafia Boxing Promotion, Matumla amewataka mashabiki wake waweze kuhudhulia pambano hilo kwani anaamini ataibuka mshindi na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

“Mpinzani wangu ajipange, maana naenda kumpiga na kuweza kuondoka na ushindi hapo kesho, na ninamuahidi kama atafika raundi ya nane, nusu ya malipo yangu nitamkabidhi maana najua hawezi kufika mpaka raundi ya nane nitakuwa nimeshamkarisha”. Amesema Matumla

Mkurugenzi wa Mafia Promotion, Ally Zayumba, akizungumza baada ya tukio hilo, amesema kutakuwa na mapambano 14 kwa mabondia wa ndani na nje ya nchi kuoneshana ubabe.

Mchakato wa kutambulisha mabondia hao lililokwenda sanjari na tambo kutoka kwa mabondia ilisababisha bondia Abdallah Pazzy ‘Dullah Mbabe’ almanusura azichape kavukavu na mpinzani wake.

Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila anatarajia kuwaongoza Watanzania kushuhudia mapambano hayo ya ngumi yasiyokuwa ya kuwania mkanda huku viongozi wengine wa Serikalini wanatarajiwa kuwepo.

Pamoja na hayo Kampuni ya Mafia Boxing Promotion imekabidhi majiko zaidi ya 30 ya gesi ya kupikia kwa mama lishe wa soko la Magomeni Jijini Dar es Salaam.









Related Posts