Coastal, Simba ugumu upo hapa!

SIMBA tayari ipo jijini Arusha kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara utakaopigwa kesho dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, huku ukionekana kuwa mgumu kwa timu zote kutokana na rekodi zilizopo mbali na matokeo ya mchezo wa awali ulioisha kwa sare ya 2-2.

Sababu kuu ya ugumu wa mchezo huo ni matokeo ambayo timu zote zimepata katika mechi za mwisho Simba ikitoka sare ya 2-2 dhidi ya Azam, huku Coastal ikitoka suluhu mbele ya Namungo, lakini nafasi ambayo kila moja ipo katika msimamo wa Ligi na pointi ambazo imekusanya hadi sasa

Simba inahitaji ushindi kesho ili ijiweke katika mazingira mazuri ya mbio za ubingwa ambapo itafikisha pointi 54, lakini itajipunguzia presha kabla ya kukutana na Yanga katika Dabi ya Kariakoo itakayopigwa Machi 8 Kwa Mkapa.

Wenyeji wa mcezo huo utakaopigwa kuanzia saa 10:00 jioni, Coastal Union inapigia hesabu za ushindi ili ifikishe pointi 27 ambazo zitaendelea kuisogeza juu kwa nafasi tatu hadi nafasi ya sita kutoka nafasi ya tisa iliyopo sasa ambapo itaishusha  JKT Tanzania kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kuna tofauti ya pointi nane tu, inayoitenganisha Coastal na timu iliyopo katika mstari wa kushuka daraja kwa sasa, lakini pointi mbili dhidi ya timu ambayo iko kwenye mstari wa kucheza playoff kubaki Ligi hivyo inalazimika kupata ushindi ili angalau iongeze pengo la pointi dhidi ya timu zilizo chini yake.

Katika mchezo wa kesho Simba itapaswa kumchunga zaidi mshambualiji wa Coastal Union, Maabad Maabad ambaye hadi sasa amepachika mabao sita hadi sasa katika Ligi Kuu.

Lakini kuna viungo wa maana kama Lucas Kikoti na Gustavo Simon ambao ndio wamekuwa Lulu la kutengeneza mashambulizi ya timu hiyo, huku wakiongezewa Rafael Daud Loth aliyetua hivi karibuni kutoka Namungo na utamu ni kutokana na ubora wao katikati ya uwanja,wachezaji wengine ni mawinga wao Bakari Bakari na Maulid Shaban.

Tishio zaidi kwa Coastal kwam kesho ni washambuliaji, Jean Charles Ahoua aliyehusika na mabao 16 ya Simba akifunga 10 sawa na aaliyonayo Clement Mzize na Prince Dube wote wa Yanga, sambamba na Leonel Ateba mwenye manane ukiachilia wakali wengine kama Kibu Denis na Ellie Mpanzu.

Hata hivyo, Simba itawakosa nyota wake wawili ambao wamekuwa na kiwango bora msimu huu mlinzi wakati Che Malone Fondoh  na kipa kinara wa clean sheat aliye na 15, Moussa Camara walioumia katika pambano lililopiga dhidi ya Azam.

Simba imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Coastallakini mara ya mwisho kukutana ilikuwa ni Oktoba 4,2024 katika mchezo wa Ligi uliopigwa kwenye uwanja wa KMC Complex ambapo timu hizo zilitoka sare ya kufungana magoli 2-2.

Simba ndio ilikuwa ya kwanza kupata goli dakika ya 25 kupitia kwa mlinzi wake Mohamed Hussein kisha mshambuliaji wake Lionel Ateba dakika ya 39 kwa mkwaju wa penati.

Kisha Coastal wakasawazisha kwa shuti za maana nje ya  18 kupitia kwa mshambualiji wake Abdallah Hassan dakika ya 47 na John kiungo Hernest Malonga dakika ya 70.

Lakini mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana jijini Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid ilikuwa ni Novemba 22,2020, Simba ikitaka kwa ushindi mnono wa mabao 7-0.

Katika mechi tano za mwisho za timu hizo zilipokutana Simba imeshinda mechi nne na sare moja mechi hizo ni Simba SC 2-2 Coastal,Okotoba 4,2024,Coastal 1-2 Simba,Machi 9,2024,Simba 3-0 Coastal,Septemba 21,2023 na Simba 3-1 Coastal,Juni 9,2023.

Katika mechi tano za mwisho za Ligi Coastal Union imeshinda moja sawa na iliyopoteza na kutoka sare mechi tatu huku Simba ikishinda tatu na kutoka sare mechi mbili.

Mechi za Coastal ni dhidi ya Namungo (0-0),Februari 23,2025,Azam FC (0-0),Februari 19,2025,Pamba Jiji FC (2-0),Februari 15,2025,Mashujaa FC (0-0),Februari 11,2025 na Jkt Tanzania (2-1),Februari 9,2025.

Mechi za Simba ni dhidi ya Azam FC (2-2),Februari 24,2025,Namungo FC (0-3),Februari 19,2025,Tanzania Prisons (3-0),Februari 11,2025,Fountain Gate (1-1),Februari  6,2025 na Tabora United (0-3),Februari 2,2025.

Kocha wa Coastal, Juma Mwambusi amefunguka kuwa mchezo huo hutakuwa mrahisi kutokana na mahitaji ya timu zote hivyo wamejipanga kuhakikisha wanabakiza pointi tatu muhimu ambazo zitawasogeza katika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

“Tuko tayari kupambana na Simba kwa sababu tunajua ubora wao upo sehemu gani na madhaifu yao pia yapo sehemu gani hivyo naamini mchezo utakuwa mzuri,” amesema Mwambusi.

Mwambusi amesema morali kwa wachezaji wa Coastal ipo juu kutokana na matokeo ambayo wamepata katika mechi mbili za mwisho wakitoka sare dhidi ya Azam na Namungo, hivyo inampa matumaini makubwa ya kuamini Leo wanaweza kushinda mbele ya Simba.

Beki wa Simba, Shomary Kapombe amesema tayari wamefanya maandalizi ya kutosha ili kushinda mchezo huo na kujitengenezea mazingira mazuri ya kutimiza malengo ambayo ni kutwaa ubingwa.

Kapombe mwenye mabao matatu na asisti tatu, amesema hakuna malengo mengine zaidi ya kushinda hivyo amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi ili kutoa sapoti ambayo itawafanya kushinda mchezo huo ambao anakiri utakuwa mgumu.

Related Posts