Moshi. Wakati upande wa utetezi ukifunga ushahidi wake katika kesi ya mauaji ya Josephine Mngara (30) aliyeuawa na kuteketezwa kwa kuchomwa moto, hukumu ya kesi hiyo inayovuta hisia za wengi, imepangwa kutolewa Machi 10, 2025.
Katika utetezi wao, washtakiwa katika kesi hiyo, Erasto Mollel na wa pili, Samweli Mchaki waliokuwa na shahidi mmoja kila mmoja, wamekana kutenda kosa hilo na kuegemea ushahidi wa kutokuwepo eneo la tukio, siku na muda lilipotokea.
Waliieleza Mahakama kuwa siku ya tukio Februari 19, 2023 walikuwa Marangu lakini Mollel alipoulizwa maswali ya dodosoo na mawakili wa upande wa mashitaka, alikubaliana na maelezo aliyoyaandika polisi.
Mshtakiwa wa pili Samweli Mchaki alikubali kumfahamu marehemu na mama yake na alishawahi kuishi na mama wa marehemu kwa miaka minane, lakini alikana kujua chochote kuhusu marehemu kuishi na mshtakiwa wa kwanza, Mollel.
Shahidi wa Mollel ambaye ni mdogo wa mshtakiwa wa kwanza, Gabriel Mongi, alimtetea ndugu yake akisema siku ya tukio, alikuwa na kaka yake Marangu wakiangalia tamthilia mpaka saa tano usiku ndipo walipoachana kwenda kulala.
Kwa upande wake, shahidi wa pili Julius Kisanga akimtetea mshtakiwa wa pili, kwa kuunga mkono ushahidi wa mshtakiwa wa pili akisema alikuwa ni mfanyakazi wake.
Aliiambia mahakama hiyo chini ya Jaji Adrian Kilimi, kuwa Februari 19,2023 alipigiwa simu na polisi wa kituo cha Polisi Himo na kutakiwa kumpeleka mshtakiwa wa pili kituoni hapo ambapo alimpeleka na kumuacha kituoni hapo.
Lakini, shahidi huyo alipoulizwa maswali ya dodoso na upande wa Jamhuri, kuhusiana na jalada lililofunguliwa polisi Februari 19, 2023, hakutaja ni kesi namba gani na kuhusu askari aliyemuita kituoni hakumtaja kwa jina mahakamani hapo.
Baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Kilimi anayesikiliza kesi hiyo alisema: – “Kesi sasa imeisha iachiwe Mahakama itafakari na kutoa maamuzi, tunatarajia hukumu itasomwa Machi 10 mwaka huu”.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Februari 24, 2025 mbele ya Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi huku upande wa mashitaka ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Kambarage Samson, Frank Ong’eng’a na Grace Kabu.
Mbali na mawakili hao, upande wa utetezi katika kesi hiyo namba 3382/2024, inayowakabili, Erasto Mollel na Samwel Mchaki, unawakilishwa na mawakili wa kujitegemea ambao ni Alfredy Sindato Silayo na Lilian Mushi.
Washtakiwa hao kwa pamoja, wanashtakiwa kwa kosa la kumuua kwa makusudi, mwanamke huyo eneo la Mtemboni, Mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Februari 19, mwaka 2023 kwa kumteketeza kwa moto.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashitaka, marehemu alikuwa akiishi na Mollel ambaye alikuwa ni mpenzi wake na aliuawa kikatili usiku wa kuamkia Februari 19, 2023 na mwili wake kuteketezwa kwa moto kwenye pagale.