Tanga. Ikiwa leo ndiyo mara ya kwanza unafika Tanga, usingeacha kujiuliza kwa msemo maarufu wa ‘Tanga ku nani?’
Sio mambo ya mahaba, bali ni mishemishe na pilikapilika za wananchi wakipita huku na kule uelekeo ni mmoja tu, katika Uwanja wa CCM Mkwakwani.
Katika uwanja huo, kunafanyika mkutano unaohitimisha ziara ya siku sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoianza Februari 23, 2025 mkoani humo.

Ziara hiyo iliyohusisha uwekaji wa mawe ya msingi na uzinduzi wa miradi mbalimbali, kadhalika kuzungumza na wananchi imehusisha wilaya zote saba za Mkoa wa Tanga.
Pia, ilijikita kuangalia namna Sh3.1 trilioni zilivyotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo za afya, barabara na maji.

Mkutano wa kuhitimisha ziara hiyo, unafanyika leo Ijumaa, Februari 28, 2025 uwanjani hapo.
Sio gari na bodaboda pekee ambazo aghalabu hushuhudiwa katika mishemishe kama hizo, waendesha baiskeli nao hawakucheza mbali.
Ile Tanga ya magari machache barabarani, leo imekuwa tofauti, ni vyombo vya usafiri vilikithiri kiasi cha kusongamana barabarani.

Ni kama hakukuwa na mwananchi aliyekubali kupitwa na tukio hilo, si mwenye kijora, dela wala kanzu na msuli, wote walifunga safari kwenda Mkwakwani.
Wengine walivalia sare za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kadhalika zilikuwepo sare nyingine za vitenge zilizonakshiwa na urembo wa maua na picha ya Rais Samia.
Kama unastaajabishwa na hayo ya nje ya uwanja, yanayoendelea ndani ya CCM Mkwakwani yatakushangaza.
Mkutano uliopangwa kuanza saa 8:00 mchana, wahudhuriaji walianza kuingia saa 1:00 asubuhi, hadi kufikia saa 5:00 asubuhi, hakukuwa na nafasi ya kuketi zaidi ya jukwaa kuu, ambalo itifaki isingekuruhusu kukaa.
Haikuwa rahisi kutofautisha idadi ya watu waliofurika ndani ya uwanja na wale waliokuwa nje wakipambana kuingia, kwa macho ya nyama idadi yao iliwiana.
Rasharasha za kuelekea saa 8:00 ya mkutano ziliongozwa na burudani za ngoma za asili na muziki wa kila aina kutoka kwa wasanii mbalimbali wakubwa wa Tanzania.
Diamond Platnumz, Marioo, Zuchu, Barobaro, Nandy, Mbosso, Samia Kings inayoundwa na Chege na wasanii wengine wengi wakiwemo wa singeli kama Sholo ‘Mwamba, Barobaro’ walikuwepo na walitoa burudani.

Kelele hazikuwa za wananchi wanaoshangilia yanayoendelea uwanjani hapo, bali vuvuzela zilipigwa pia.