AZAM FC juzi usiku ililazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na Namungo, ikikamilisha mechi ta tatu mfululizo bila kuonja ushindi.
Azam ilianza na suluhu na Coastal Union, kisha kupata sare ya 2-2 na Simba kabla ya juzi tena kubanwa nyumbani na Namungo baada ya Gibril Sillah kufunga bao la kusawazisha dakika chache kabla ya mapumziko. Namungo ndio ilitangulia kupata bao la mkwaju wa mbali wa Hamis Khalifa ‘Nyenye’ dakika ya 12 na kuifanya Azam katika mechi hizo tatu zilizopita kuzitema pointi sita na kusalia na kufikisha 45 ikibaki nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara unaoongozwa na Yanga.
Mara ya mwisho Azam kucheza mechi tatu mfululizo bila kushinda ilikuwa Desemba 2022, wakati Kally Ongala akiwa kaimu kocha mkuu.
Chini ya Kally, Azam ilitoka sare ya 2-2 ugenini dhidi ya Kagera Sugar, kisha 1-1 na Geita Gold pia ikiwa ni ya ugenini na kuja kupasuka nyumbani kwa mabao 3-2 kutoka kwa Yanga.
Hata hivyo, Azam ya Kali Ongala ilitoka kushinda mechi nane mfululizo kabla ya mechi hizi tatu.
Lakini Azam ya Rachid Taoussi imetoka kubaya zaidi kwani katika mechi tano zilizopita imeshinda mechi moja tu.
Ilipasuka 1-0 kwa Pamba Jiji ikiwa ugenini, ikashinda nyumbani 2-0 dhidi ya Mashujaa kabla ya kuambulia sare hizo tatu mfululizo, mbili za ugenini na moja ya nyumbani.
Hakuna namna yoyote ya kuyaelezea matokeo haya zaidi ya kusema kocha Taoussi amefeli.
Chini ya kocha huyu raia wa Morocco, Azam imecheza mechi 21, ikishinda 13, ikipoteza tatu na sare tano.

Kwa kulinganisha na msimu uliopita ikiwa chini ya Yousouph Dabo, Azam ya Rachid Taoussi imefeli sana msimu huu.
Chini ya Dabo, Azam ilimaliza na pointi 69 ambazo ni za juu zaidi katika wakati wote ambao ligi imekuwa na timu 16…mechi 30 kwa msimu.
Msimu pekee ambao Azam ilipata alama nyingi zaidi ya hizo ulikuwa ule wa 2019/20 ambao ilipata alama 70, hata hivyo huo msimu ulikuwa na timu 20…mechi 38 kwa msimu.
Chini ya Taoussi, hadi sasa Azam ina pointi 45 na zimebaki mechi nane. Ili kufikia alama za msimu uliopita, Azam inapaswa kushinda mechi zote nane zilizobaki.
Msimu uliopita katika idadi kama hiyo ya mechi 22, Azam ilikuwa imeshinda mechi 15, sare tano na kupoteza michezo miwili tu dhidi ya Yanga na Namungo na ikavuna jumla ya pointi 50.
Kinyume na hapo itakuwa imevuna alama chini ya 69 na kudhihirisha kufeli kwa Rachid Taoussi.
Kwa mwenendo huu kusuasua wa Azam ya Taoussi, nafasi ni finyu sana kushinda mechi zote nane zilizobaki.

Chini ya Yousouph Dabo, hadi mzunguko wa 22 kama sasa, Azam FC ilikuwa imeshafunga mabao 54.
Suala la kupata mabao kwa Azam FC halikuwa gumu kwani yalikuja kutoka kila upande.
Lakini chini ya Taoussi, Azam hadi mzunguko wa 22 imefunga mabao 32 tu.
Azam inahangika sana, sio tu kufunga, bali hata kutengeneza nafasi.
Chini ya Dabo, Azam ilikuwa timu nzuri ya kuitazama ikicheza. Ilikuwa na utambulisho wake unaivutia.
Kwa makocha wa timu pinzani, Azam ya Dabo ilikuwa jinamizi kukutana nayo.
Kasi ya mchezo na usahihi wa matukio ulikuwa wa hali ya juu sana.
Lakini chini ya Taoussi, Azam haivutii kuiangalia. Haichezi mpira mzuri na wala haitishi wapinzani.
Haina utambulisho wake na wala huoni mbinu zaidi ya uwezo binafsi wa wachezaji.

4. Maendeleo ya wachezaji
Chini ya Dabo, wachezaji wa Azam waliimarika sana mmoja mmoja.
Mbinu ya ‘invented full back’ yaani walinzi wa pembeni kuchezea ndani kidogo na kuwaacha mawinga kutamba pembeni zaidi iliwafanya Pascal Msindo na Lusajo Mwaikenda kuwa wachezaji hatari sana.
Ni katika kipindi hicho ndipo tuliposhuhudia wachezaji hawa wakifunga mabao kama washambuliaji na wakitoa pasi za usaidizi wa mabao kama viungo wachezeshaji.
Viungo kama Yahya Zayd, Adolf Mtasingwa, Sospeter Bajana na hata Feisal Salum walikuwa katika sayari yao ya tofauti kabisa.
Lakini chini ya Taoussi wachezaji wengi wamekwama…hawatishi tena.
Hakuna anayemjadili tena Yahya Zayd wala Mtasingwa, zaidi ya mazoea ya msimu uliopita.
Wachezaji wengi chini ya Taoussi wameshuka viwango na kilichobaki kwao ni jitihada tu.
Mchezaji kama Idd Seleman ‘Nado’ ambaye kwa Dabo hakuwa akipata sana nafasi, lakini akikuwa hatari zaidi kuliko sasa ambako anacheza kila siku.

Tatizo kubwa kwa miaka mingi kwa wachezaji wa Azam FC ni kuonekana kama hawana njaa ya kufanikiwa, lakini chini ya Dabo ilianza kuwa tofauti.
Chini ya Yousouph Dabo wachezaji wa Azam walianza kujenga utamaduni mpya wa kuipigania timu.
Timu ilicheza kwa ari ya hali ya juu na kulazimisha matokeo katika hata kwenye uwanja mgumu.
Lakini chini ya Taoussi hali imebadilika. Wachezaji wa Azam ni kama wamepoteza hamu ya kuichezea timu.
Hawalazimishi tena matokeo kama awali. Wanacheza kama watu wasiotafuta kitu zaidi ya kusubiri mpira uishe waende kwenye vitu vyao vya maana kuliko hiyo mechi.
Baada ya sare dhidi ya Namungo, Rachid Taoussi aliwalaumu wachezaji wake kwa kukosa umakini wa mchezo.
Alisema kwamba walicheza kwa kuridhika sana kufuatia sare dhidi ya Simba.
Hii si kweli, namna ambavyo walicheza dhidi ya Namungo ndio vile vile walicheza dhidi ya Mashujaa au KMC, kwa mechi za Chamazi mwaka huu 2025.
Taoussi asiisingizie mechi ya Simba imewalevya wachezaji wake, hapana.
Hiki ndicho kiwango cha timu yake kwa sehemu kubwa ya msimu ya msimu huu.
Na kuna mechi ambazo timu yake imecheza chini ya kiwango hicho.
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wana msemo wao wa fundi mbovu husingizia vifaa vyake.
Hiki ndicho ninachokiona kwa Taoussi. Ameanza kusingizia wachezaji wake ilhali matatizo makubwa zaidi ni mbinu zake na siyo uwezo au umakini wa wachezaji wake.

Rachid Taoussi alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Azam, kama kweli wanataka kusonga mbele… waachane naye baada ya msimu kuhitimika.
Sio kwamba Taoussi ni kocha mbaya, hapana…ila ujenzi wa Azam umemshinda.
Aina yake ya mpira haiwezi kuitoa Azam hapo ilipo na kwenda mbele, zaidi itashuka chini.
Azam ya Rachid Taoussi imerudi kwenye zile za kabla ya Yousouph Dabo, ambazo sifa yake ilikuwa kushindana na timu ya nne.
Kwa msimu huu vita ya Azam ni dhidi ya Singida Black Stars kuwania nafasi ya tatu, sio tena Yanga au Simba kuwania nafasi ya pili au ya kwanza kama msimu uliopita chini ya Dabo.
Huku ni kurudi nyuma na haifai kwa timu kama Azam.