Mahakama yahalalisha uchaguzi mitaa mingine minne Kigoma

Kigoma. Mahakama ya Wilaya Kigoma imehalalisha uchaguzi wa wenyeviti wa mitaa minne katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, baada ya kutupilia mbali mashauri ya kupinga uchaguzi katika mitaa hiyo uliofanyika Novemba 27, 2024.

Hukumu hizo zimetolewa Alhamisi Februari 27, 2025 na mahakimu wawili tofauti waliosikiliza mashauri hayo kwa nyakati tofauti, baada ya kukataa madai na hoja za walalamikaji.

Mahakama imesema mmoja wa walalamikaji hakuwa mgombea katika mtaa aliokuwa akipinga uchaguzi huo.

Mitaa iliyolalamikiwa inayohusika na hukumu hizo ni Kibirizi, Kata ya Kibirizi, Mtaa wa Busomero (Kata ya Kasimbu), Mtaa wa Livingstone (Kata ya Kasingirima) na Mtaa wa Lake Tanganyika (Kata ya Buzebazeba).

Mahakimu hao wamesema walalamikaji wameshindwa kuthibitisha madai yao kwa kiwango kinachotakiwa, pamoja na mambo mengine hawakuwasilisha ushahidi wa nyaraka na hawakuita baadhi ya mashahidi, hasa mawakala au wapigakura wengine kuunga mkono madai yao.

Kutokana na kasoro zilizoainishwa, mahakimu hao wamesema yote yaliyofanyika katika uchaguzi huo kwenye mitaa hiyo ni sahihi na yanabaki kama yalivyo, isipokuwa kama yatatenguliwa na ngazi ya juu ya Mahakama, ikiwa walioshindwa watakata rufaa.

Mashauri hayo yalifunguliwa na wanachama wa ACT- Wazalendo, waliogombea nafasi za uenyekiti katika mitaa hiyo wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji wa mwaka 2024 dhidi ya wenyeviti wa mitaa waliotangazwa kuwa washindi katika mitaa hiyo, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiwa wajibu maombi (walalamikiwa) wa kwanza.

Waliofungua mashauri hayo ni Didasi Baoleche aliyegombea Mtaa Kibirizi dhidi ya Mrisho Mwamba wa CCM aliyetangazwa mshindi.

Khalfan Nyunya, aliyegombea katika Mtaa wa Busomero alifungua kesi dhidi ya Hassan Omary wa CCM.

Mashauri hayo mawili yalisikilizwa na kutolewa hukumu na hakimu Anna Kahungu.

Wengine waliofungua mashauri ni Luma Akilimali, aliyegombea mtaa wa Livingstone dhidi ya Mawazo Kiembe wa CCM na Kamongo Frank aliyegombea Mtaa wa Lake Tanganyika dhidi ya Mohamed Nusura wa CCM.

Mashauri hayo yalisikilizwa na kutolewa uamuzi na hakimu Aristida Tarimo.

Walalamikiwa wengine katika mashauri hayo ni wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya mitaa katika mitaa inayolalamikiwa na msimamizi wa uchaguzi, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji (ambaye ni mkurugenzi wa manispaa hiyo).

Walikuwa wakipinga mwenendo na matokeo ya uchaguzi wakidai ni batili kwa kuwa haukuwa huru na wa haki kutokana na kasoro walizosema zilijitokeza kabla, wakati na baada ya upigaji kura.

Kasoro hizo walisema ni ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi zilizowekwa katika upigaji kura, kuhesabu na kutangaza matokeo. Pia kuwepo kwa kura bandia zilizoingizwa katika masanduku ya kura isivyo halali.

Katika mitaa mingine walisema kulitokea vurugu zilizosababisha kura kutohesabiwa lakini baadaye wagombea wa CCM wakatangazwa washindi.

Madai mengine yalikuwa uwepo wa kura bandia ambazo baadhi ya wapigakura katika baadhi ya vituo walikamatwa nazo na nyingine zikaingizwa katika masanduku na watumishi wa Serikali na mtendaji wa kata.

Walidai uwepo wa kura bandia ulisababisha tofauti ya idadi ya kura zilizopigwa kati ya nafasi ya uenyekiti wa mtaa na nafasi za wajumbe.

Waliiomba mahakama itamke uchaguzi katika mitaa hiyo ni batili, iwaamuru wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa mitaa hiyo watangaze uchaguzi ndani ya siku saba au 14 na kufanya uchaguzi mwingine ndani ya siku 60.

Mahakimu hao katika hukumu wamekataa madai yote ya walalamikaji wakisisitiza hawakuyathibitisha, ikiwemo kuwasilisha mahakamani kura bandia, wala wengine kueleza idadi.

Katika shauri la Mtaa wa Kibirizi (Baoleche dhidi ya Mwamba) hakimu Kahungu amesema baada ya kuangalia ushahidi ameridhika kuwa mlalamikaji, Baoleche hakuwa mgombea wa nafasi hiyo katika uchaguzi huo.

Kahungu amekubaliana na madai ya mlalamikiwa wa pili, aliyekuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa huo aliyekana kuwa hakuwahi kumteua.

Mlalamikiwa wa kwanza, Mwamba (aliyetangazwa mshindi) alieleza katika ushahidi kuwa Baoleche alikuwa mgombea mwenzake, pia Baoleche aliwasilisha mahakamani baadhi ya fomu za matokeo ya mwenyekiti ambazo jina lake lilikuwapo, ambazo zilipokewa kama kielelezo cha ushahidi wake.

Hakimu Kahungu ingawa hakuzungumzia kielelezo hicho, katika uamuzi amesema mlalamikaji hakuwa mgombea kwa kuwa hakuwasilisha mahakamani barua ya uteuzi ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa kuthibitisha kuteuliwa kwake.

“Kwa kuwa kesi haikuthibitishwa matokeo yaliyopo yanabaki kama yalivyo isipokuwa kama yatatenguliwa na ngazi nyingine,” amesema hakimu Kahungu baada ya kujadili ushahidi na madai ya mlalamikaji katika shauri hilo la Baoleche na kuhitimisha:

“Hivyo mahakama hii haiwezi kuvuruga matokeo yaliyotangazwa na madai ya mlalamikaji hayana mashiko na maombi haya yanatupiliwa mbali kwa gharama.”

Wakizungumzia hukumu hizo, mawakili waliowawakilisha walalamikaji, Eliutha Kivyiro na Prosper Maghaibuni wamesema uamuzi wa Mahakama hiyo siyo wa mwisho.

“Tutajadiliana na wateja wetu kwa ajili ya kukata rufaa ngazi ya juu,” amesema Kivyiro.

Wanachama wa ACT-Wazalendo waliofika mahakamani kusikiliza hukumu hizo akiwamo Katibu Mkoa wa Kigoma, Yunusa Ruhomvya amesema hawajaridhika na uamuzi huo na watakwenda mpaka Mahakama ya Rufani.

Hukumu za mashauri hayo manne ni miongoni mwa  saba yaliyosikilizwa mpaka mwisho kati ya tisa yaliyofunguliwa na chama hicho katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, baada ya mashauri mawili kuondolewa kwa sababu za kiufundi kutokana na pingamizi za walalamikiwa.

Februari 24, mahakama hiyo ilitoa hukumu za mashauri mengine matatu yaliyosikilizwa na mahakimu wawili tofauti. Mahakama ilihalalisha uchaguzi katika mtaa mmoja na kijiji kimoja.

Katika hukumu ya shauri la Mtaa wa Gezaulole, Kata ya Gungu lililofunguliwa na Lovi Omary, iliyotolewa na hakimu Katoki Mwakitalu, ilibatilisha uchaguzi na kutengua ushindi katika mtaa huo baada ya kuridhika kuwepo ulaghai na kura bandia.

Walalamikaji katika mashauri hayo saba waliwakilishwa na mawakili Thomas Msasa (kiongozi wa jopo), Kivyiro na Maghaibuni.

Related Posts