Maji ya Ziwa Victoria kuokoa ndoa, mimba za utotoni Ushetu

Kahama. Wananchi zaidi ya 180,000 wa Halmashauri ya Ushetu wanaotumia maji ya visima na kwenye madimbwi wako mbioni kuondokana na adha hiyo, baada ya Serikali kutoa zaidi ya Sh44 bilioni kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria.

Mradi huo pia utaondoa vifo vya watoto wanaogelea kwenye madimbwi wanapokwenda kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

 Mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao tayari umetekelezwa Kahama, utatekelezwa kwenye Halmashauri ya Usheru kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ikitarajiwa kuhudumia kata 11 kati ya 20 na vijiji 54 kati ya 112 vya Ushetu .

Wakizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Februari 28, 2025 baadhi ya wanawake wa Ushetu wamesema ukosefu wa maji katika maeneo yao unawafanya kutumia ya visima na madimbwi, kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ambayo siyo safi na salama, lakini pia yanahatarisha maisha ya watoto wao wanaooga maeneo hayo.

“Hatuna maji kwa hiyo lazima watoto na hata mabinti zetu wakaoge na kufua kwenye visima na wakati mwingine kwenye madimbwi. Kuna madhara wakienda huko ikiwemo kuzama na mimba kwa mabinti zetu,” amesema Agnes Malunde mkazi wa kijiji cha Mbika.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Chanda Msogoti amesema  hulazimika kuamka saa tisa usiku kwenda kutafuta maji na kuwaacha waume zao kitandani, na wanapochelewa  kurudi huzua mgogoro  kutokana na wenzi wao kutoamini kama walikuwa kwenye kutafuta maji.

“Hali ya ndoa kwa wanaume zetu mbaya sana, maana kuamka ile saa tisa ya usiku, anahisi kama unatoka kwenda sehemu nyingine kumbe unafuata maji, huu mradi utatusaidia sana kwa kweli” amesema Msogoti

 Mbunge wa Ushetu, Emanuel Cherehan ameishukuru Serikali kwa mradi huo, huku akieleza kuwa utakuwa suluhu ya kudumu ya changamoto ya maji kwa wakazi wa Ushetu, iliyowatesa kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu, Gagi Lala ameomba kuharakishwa kwa upanuzi wa mradi huo ili vijiji vyote 112 viweze kufikiwa na huduma ya maji safi na salama kutoka  ziwa hilo.

Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Shinyanga, Julieth Payovela akizungumza wakati wa hafla  ya kukabidhi mabomba kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, Februari 23 mwaka huu alisema, kukamilika kwa mradi kutapunguza adha ya magonjwa ya mlipuko iliyokuwepo pamoja na kupunguza ndoa na mimba za utotoni kwa wanafunzi wa kike.

“Mradi huu utahudumia zaidi ya wananchi 189,000 wa kata hizo 11, utasaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko, mimba za utotoni na utoro wa wanafunzi mashuleni, lakini pia utaondoa kero kwenye ndoa nyingi” alisema Payovela

 Alisema mradi huo utakamilika Oktoba 2026 kwa gharama ya zaidi ya Sh44 bilioni.

Related Posts