Makosa hatari ya kitabibu kwa wagonjwa wodini

Dar es Salaam. Wagonjwa wenye mahututi walio wodini, wako hatarini mara saba zaidi kupoteza maisha kwa kukosa huduma za msingi, utafiti umebaini.

Imebainika kuwa asilimia 69 ya wagonjwa mahututi tofauti na dhana iliyojengeka, walikuwa wakitibiwa katika wodi za kawaida na sio wodi za uangalizi maalum  (ICU).

Kufuatia matokeo hayo, wataalamu wa afya wamesema endapo madaktari watafuata hatua 40 muhimu za vipimo, ikiwemo kupima mara kwa mara joto la mwili, shinikizo la damu, kiwango cha hewa safi kinachoingia kwenye mapafu, kutasaidia kuondoa hatari hiyo.

Matokeo ya utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili, Muhas kwa kushirikiana na watafiti wa Apprise, uliochapishwa katika jarida la Lancet leo Alhamisi, Februari 27, 2025,  uliangazia tatizo la hali ya umahututi na fursa ya kuokoa maisha kwa gharama nafuu katika hospitali za Afrika.

Utafiti huu uliofanyika katika nchi 22 barani Afrika ikiwemo Tanzania, ni wa kwanza kutoa tathmini ya kina kuhusu uwepo na ukubwa wa tatizo la hali ya umahututi pamoja vifo vitokanavyo na wagonjwa mahututi barani Afrika.

Kitaalamu hali hii ya umahututi huwa na uwezekano wa kutengamaa, endapo huduma sahihi itatolewa haraka na kwa njia sahihi.

Akizungumza na Mwananchi, Dk Isaac Maro amesema tafiti zinaonesha, watumishi wa afya wakizingatia kanuni 40 za kumfuatilia mgonjwa kwa kutumia vipimo vya kawaida walivyofundishwa na kuvitumia vyuoni, wanaweza kuzuia mgonjwa aliye wodini asipelekwe chumba cha dharura.

“Utaratibu huo una vipimo 40 ikiwemo joto la mwili, shinikizo la damu, kiwango cha hewa safi kinachoingia kwenye mapafu. Ni vipimo ambavyo vipo kwa kawaida na kila mmoja anavitumia kwa wanaotoa huduma za afya.

“Wengi hudharau hivyo vipimo, havifanyiki. Kwa mfano,  kuna mgonjwa wodini mara nyingi anapimwa wakati  daktari anapozunguka wodini  na vile atakavyotaka vifanyike baadaye. Hapo  katikati anaweza kuzidiwa na wapo wanaopoteza maisha,” amesema Dk Maro.

Amesema daktari akiingia wodini, ana uwezo wa kugundua wagonjwa ambao hali zao zinabadilika kwa kutumia tu vipimo vya kawaida vya kupima joto la mwili.

“Ukimpima kila baada ya saa nne, utaguundua mgonjwa anapandisha homa mapema kabla haijamletea shida, kama unapima presha kila baada ya muda unaotakiwa,  una uwezo wa kugundua kuwa shinikizo la juu la damu la mgonjwa linaongezeka,” amesema.

Dk Maro amesema iwapo madaktari na watumishi wote wa afya,  watatumia mbinu zote walizofundishwa, wataokoa wagonjwa wengi.

“Si hivyo tu tunapoteza fedha nyingi kuhudumia wagonjwa ambao wameshazidiwa. Tuna uwezo wa kutambua wagonjwa walio katika hali mbaya na kuepusha dharura siyo maeneo yote au mikoa yote ina hospitali zenye ICU,” amefafanua.

Utafiti huo uliohusisha wagonjwa 19,872 watu wazima kuanzia miaka 18,  umeonesha wagonjwa wengi mahututi, hupoteza maisha kwa sababu kuna huduma muhimu za msingi ambazo hazitolewi au hazizingatiwi kwa wagonjwa waliolazwa katika wodi za kawaida.

Sehemu ya utafiti huu imebainisha asilimia 12.5 yaani mtu mzima mmoja kati ya wanane waliolazwa hospitalini, ana hali ya umahututi. Matokeo haya yanaonesha ukubwa wa tatizo na namna linavyopaswa kupewa kipaumbele.

Sehemu ya matokeo ya utafiti yalionesha asilimia 21 ya wagonjwa mahututi , walifariki ndani ya siku saba hospitalini, ikilinganishwa na asilimia 2.7 ya wagonjwa wasio mahututi.

Kwa tafsiri nyingine ni kuwa mgonjwa mwenye hali ya umahututi uwezekano wake wa kupoteza maisha ndani ya siku saba,  ni karibu mara saba zaidi ya yule asiye na hali ya umahututi.

Kwa kuwa hali ya umahututi inaweza kusababishwa na ugonjwa wowote ule kama malaria, magonjwa ya kuhara, magojwa ya moyo, saratani na mengineyo,  utafiti huu unafumbua macho juu ya umuhimu wa huduma kwa wagonjwa mahututi kupatikana sehemu zote.

Watafiti hawa, ambao pia ni vinara katika vuguvugu la upatikanaji wa ‘tiba okovu na huduma ya msingi kwa wagojwa mahututi,’  wamebaini kuwa na asilimia 69 ya wagonjwa mahututi, tofauti na dhana iliyojengeka, walikuwa wakitibiwa katika wodi za kawaida na sio wodi za uangalizi maalum (ICU).

Utafiti huu unaonesha uwepo wa pengo kubwa katika utoaji wa huduma okovu za misingi na za gharama nafuu, ambapo zaidi ya nusu ya wagonjwa mahututi (asilimia 56) hawakuwa wakipata huduma hizi rahisi wanazohitaji, kama vile oksijeni kwa kushindwa kupumua au dripu ya kusaidia mzunguko wa damu.

Kiongozi wa utafiti huo, Profesa Tim Baker amesema pengo hili la huduma za msingi linaashiria uwezekano mkubwa wa kuokoa maisha ya wagonjwa wengi mahututi, wanaolazwa kwenye wodi za kawaida.

“Matokeo haya yanapaswa kubadilisha mtazamo wetu kuhusu huduma za wagonjwa mahututi. Bara la Afrika linakabiliwa na mzigo mkubwa zaidi wa wagonjwa mahututi kuliko tulivyodhani hapo awali,” amesema.

Amesema kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza vifo vinavyotokana na wagonjwa mahututi, ikiwa tu huduma za msingi, rahisi na za gharama nafuu kwa wagojwa zitatolewa ipasavyo.

Jopo la watafiti hao akiwemo Dk Karima Khalid liko mbioni kufanikisha mradi mkubwa wa kuongeza upatikanaji wa tiba okovu na huduma ya msingi kwa wagojwa mahututi, katika vituo vya afya ya msingi katika baadhi ya mikoa ya Tanzania bara na visiwani.

Mradi huu unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia Tamisemi na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la  Watoto (Unicef).

Related Posts