SIMBA ya msimu huu chini ya Kocha Fadlu Davids imeonekana moto, ikiusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kulikosa kwa misimu mitatu mfululizo, lakini ikiwa timu pekee iliyosalia katika michuano ya CAF ikitinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba iliyocheza mechi 20 ikikusanya pointi 51, ikiwa imefunga mabao 43 na kufungwa nane tu ikiwa ndio yenye ukuta mgumu, lakini siri ya mafanikio hayo imefichuliwa na nyota wa timu hiyo hasa wanapokuwapo kambini kujiandaa na michezo yao iwe ya ndani au ile ya kimataifa.
Hakuna aliyekuwa anajua juu ya siri kubwa inayoendelea katika kambi ya Simba katika kuhakikisha inapambania ubingwa kwa jasho na damu, huku kocha wa timu hiyo akibariki kila kitu.

Siku moja kabla ya mechi ya Simba dhidi ya Azam, iliyopigwa Jumapili na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 Uwanja wa Benjamin Mkapa, mastaa wa Wanamsimbazi walionekana wakicheza muziki wakiwa na redio kama moja ya kujiweka sawa kiakili, jambo ambalo hawakuonekana wakilifanya hapo awali.
Wakongwe katika kikosi hicho, nahodha Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na beki Shomari Kapombe, walifichua wanachokifanya kambini kinachowasaidia kuendelea kukaa katika morali na ari ya mchezo itakayowasaidia kuwania ubingwa kwa msimu huu.
Tshabalala ndiye aliyenunua redio hiyo ni utaratibu wake kufungulia muziki na kucheza kambini, huku wakitajwa vinara wa kumuunga mkono na kupenda kucheza ni Leonel Ateba anayemiliki mabao manane na Fabrice Ngoma.

Tshabalala alisema kazi wanayoifanya ni ngumu ndiyo maana aliona njia sahihi ya kujiweka sawa kiakili ni kusikiliza muziki na kucheza na ameona ni jambo linalowafanya liwaweke pamoja na kujuana kitabia pia wanapata muda wa kuambiana majukumu uwanjani.
“Ni kawaida yetu kambini kufanya hivyo, mfano inaweza ikatokea tukapata matokeo mabaya tofauti na matarajio yetu na mbele yetu kuna mechi, lazima tujiweke sawa kiakili kuhakikisha tunakuwa morali ya kupambania ushindi ili tuweze kufikia malengo yetu ya kuchukua ubingwa msimu huu,” alisema Tshabalala na kuongeza;
“Sio jambo geni mfano kama Afrika Kusini na Ulaya, wachezaji unawakuta wanapoingia uwanjani, wakiwa kwenye gari la timu ama wametulia maeneo unawaona wanasikiliza na wengine muziki na wengine wanacheza hiyo kwao ni tiba ya kukaa sawa kiakili.”

Kwa upande wa Kapombe alisema Tshabalala ndiye kinara wa kufanya mambo hayo anapenda kumuona kila mchezaji anakuwa na furaha kabla na baada ya mechi, lakini alikiri ni kitu kizuri.
“Tshabalala ndiye mwenye hiyo redio, anapenda sana mambo ya muziki na kuona kila mtu anakuwa na furaha ili kujijengea kujiamini zaidi, inasaidia kujuana kitabia, binafsi napenda uwepo wake katika timu kuna kitu anakiongeza kwa wachezaji wenzake kuwa wazalendo kwa ajili ya Simba na ikikosekana unajua kabisa,” alisema Kapombe aliyefunga mabao matatu na asisti tatu mechi za Ligi Kuu.
Kocha Fadlu, alisema hawezi kuwakataza mastaa wa timu hiyo kufanya hivyo kwa sababu ameona ni kitu kinachowaweka sawa kiakili na ni kitu cha kawaida nchini kwao Afrika Kusini, kuwaona wachezaji wanacheza na kusikiliza muziki.
“Lingekuwa ni jambo linaloharibu kazi ningeishalizuia, kinachofanyika kinawasaidia wachezaji kujuana zaidi na kuwaweka pamoja pia nawaona wanahamasishana kuhusu kazi, ndio maana umeona juzi katika mazoezi walikuwa wanacheza ili kujijengea kujiamini zaidi kwa mchezo ambao ulikuwa mbele yao,” alisema kocha huyo na kuongeza;

“Mchezaji anafanya kazi ngumu lazima akili yake iwe tayari muda wote na awe na furaha, kama kocha napenda kuwaona wanafurahia pamoja, itakuwa rahisi kuwania ubingwa kwa umoja na nguvu moja.”
Kikosi cha Simba kesho kinatarajiwa kuwa wageni wa Coastal Union katika pambano jingine la Ligi Kuu kabla ya kuigeukia Dabi ya Kariakoo itakayopigwa Machi 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.