Katika kuhakikisha kikosi chake kinaendelea kukaa kileleni kwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Yanga, Hamdi Miloud amesema wamekuja Mwanza kwa ajili ya kushinda na kupata alama tatu na sio matokeo mengine yoyote ambayo yatawapunguza kasi.
Yanga ambao ni vinara wa Ligi Kuu ikiwa na alama 55 katika mechi 21 ipo jijini Mwanza na leo jioni itamenyana na Pamba Jiji yenye alama 22 katika nafasi ya 12, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Yanga imeendelea kujihakikishia nafasi ya kuongoza ligi hiyo baada ya washindani wao wa karibu katika mbio za ubingwa, Simba kuangusha alama juzi kwa kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Azam FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi hicho, Miloud amesema wanatambua mechi dhidi ya timu aina ya Pamba Jiji zinazopambana zisishuke daraja huwa ni ngumu lakini wamekuja kwa kazi moja tu ya kushinda mechi hiyo.
“Mchezo wa Pamba ni kama mechi nyingine tunahitaji kushinda na kuchukua pointi tatu ambazo ni muhimu sana kwetu, tunapocheza na timu za ina hii tunahitaji kuwa makini zaidi na wastahimilivu sisi ni Yanga tunahitaji kushinda kila mchezo,” amesema Miloud na kuongeza;
“Hivyo, lazima tuwe makini zaidi kuhakikisha lengo hilo linatimia, kesho ni mechi ngumu kwa sababu kila mmoja katika klabu yetu ana mategemeo hayo tunashukuru na kuwapongeza mashabiki wetu kwa namna wanavyotupa nguvu ya kupambana ni motisha kubwa ya kuendelea kusukuma zaidi kufikia malengo na kuwapa furaha.”
Mchezaji wa timu hiyo kutoka timu ya vijana, William Chigomba amesema kwa sasa hawaangalii mpinzani wao Simba anafanya nyinyi bali wanazingatia alama tatu katika mechi zao huku wakiacha kila timu icheze mechi zake.
“Cha msingi pointi tatu ili kuendelea kuwa kileleni dhidi ya wapinzani wetu ambao ni Simba tunaangalia nafasi yetu zaidi kwenye ligi hivyo hivyo tunapaswa kuhakikisha tunaendelea kushinda ili tusitoke tulipo. Wapinzani wetu Pamba ni timu nzuri na sisi tulio kwenye mbio za ubingwa hakuna mechi rahisi,” amesema Chigomba.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Oktoba mwaka jana, Pamba ilifungwa mabao 4-0 na Yanga na hivyo leo itakuwa na kazi ya kulipa kisasi sambamba na kukusanya pointi za kuwaweka salama katika msimamo wa Ligi Kuu inayomalizia raundi ya 22.