Miradi 10 yapata ruzuku ya utafiti kuondoa umaskini

Dar es Salaam. Miradi 10 ya utafiti nchini Tanzania imepata   ruzuku ya  utafiti chini ya mfuko wa DEEP Challenge Fund unaotoa fedha kwa watafiti wanaokusanya data, taarifa na takwimu za hali ya umaskini na kutoa njia za kukabiliana na hali hiyo.

Mfuko huu uliozinduliwa Machi 2024 unatekelezwa na shirika la Oxford Policy Management Tanzania, ukilenga kuwezesha watafiti wa Kitanzania kujifunza njia za kisasa za ukusanyaji taarifa, ushahidi wa kisayansi na takwimu zinazoweza kutumika kupima umaskini.

Mkurugenzi Mkazi wa shirika hilo, Dk Charles Sokile amesema kupitia mfuko huo watafiti wa Tanzania watafanya tafiti zitakazoweza kupima umaskini kwa haraka, muda mfupi na gharama nafuu kwa kutumia teknolojia ikiwemo akili bandia na data kubwa.

“Njia nyingi tulizonazo za kupima umaskini huwa ni gharama na zinachukua muda mrefu inaweza kuwa baada ya miaka 10 nikitolea mfano sensa. Tumekuja na njia mbadala ambazo zinaweza kupima umaskini kwa haraka.

“Tumeshazifanyia utafiti njia hizi za kukusanya takwimu na tumejiridhisha kuwa licha ya kuwa inaweza kutoa majibu ndani ya muda mfupi ufanisi wake ni asilimia 80 ya njia zile za muda mrefu kama sensa,”amesema 

Amesema kwa kutumia njia hizo watafiti wa Tanzania wataweza kushirikiana na wataalamu wengine kupima umaskini na kutoa takwimu ambazo zitafanya sera za Serikali ziweze kusaidia watu wengi kujikwamua kwenye umaskini.

Mshauri mwandamizi na wa shirika hilo, Pamela Shao amesema baada ya mfuko huo kuzinduliwa maombi ya miradi 154 yalipokelewa kutoka kwa watafiti na taasisi za utafiti na kati ya hiyo miradi 10 ndiyo imefanikiwa kupata ruzuku kati ya paundi 5,000 sawa na  Sh13.7 milioni hadi paundi 50,000 sawa na Sh150 milioni.

“Kila mradi ambao umefanikiwa kupata ruzuku umeonesha ni namna gani utaleta matokeo kwenye mkakati wa kukabiliana na umaskini hapa nchini . Tuna kila sababu ya kuwashukuru watafiti na taasisi ambazo zimewasilisha miradi yao na waliofanikiwa kushinda tunasubiri kwa hamu kuona matunda yatakayoletwa na tafiti wanazoenda kufanya,” amesema Pamela.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Dk Rahma Mahfoudh amesema Serikali inafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa dhamira ya kutokomeza umaskini nchini.

“Imani yetu ni kwamba watafiti hawa watatumia ruzuku walizopata kwenda kufanya tafiti katika maeneo yaliyolengwa, hapa tunachotaka ni kuona matokeo yanatufikisha kwenye lengo letu la kutokomeza umaskini. Hili litafanyika kupitia matokeo ya kisayansi yatakayoletwa na watafiti wetu,” amesema Dk Rahma.

Related Posts