MUHAS Yazindua Mfuko wa Wakfu wa Ali Hassan Mwinyi.

Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi, Dkt Hussein Mwinyi amekipongeza Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kuanzisha Mfuko wa Wakfu wa Ali Hassan Mwinyi kwani itasaidia kujenga, kutekeleza miradi na kupunguza utegemezi kutoka Serikalini.

Amesema fedha zitakazopatikana kutokana na mfuko huo zitasaidia mahitaji ya chuo hicho,udhamini wa wanafunzi pamoja na tafiti.

Dkt. Mwinyi amesema hayo Leo Februari 28,2025 wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa Ndaki ya Tiba, Kampasi ya Mloganzila, uzinduzi wa Mfuko wa Wakfu wa Ali Hassan Mwinyi (AHMMEF) na kongamano la kumuenzi Rais Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Mkuu wa wa kwanza wa chuo hicho na Rais wa pili wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania.

“Nimefarijika chuo kuanzisha kongamano la kila mwaka la kuenzi mchango wa Mkuu wa chuo wa kwanza, natambua kwamba makongamano haya yanakutanisha wanasayansi, watafiti, watunga sera na wadau wa maendeleo,” amesema Rais Mwinyi.

Amesema sekta ya afya inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa wataalamu wenye ujuzi wa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na ya kuambukiza.

Aidha, amesema vifo vya mama na mtoto bado vimeendelea kuwa juu licha ya kiwango chake kushuka kutoka 578 katika vizazi hai 100,000 hadi 104 katika vizazi hai 100,000 hivyo jitihada zinatakiwa kukabiliana na hali hiyo.

Amesema mabadiliko ya tabia nchi na mfumo wa maisha umechangia kuwepo kwa magonjwa mengi ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza hivyo kama Taifa hawana budi kuwekeza.

“Sekta ya elimu ina mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya wataalamu wa tiba, utafiti na ubunifu sambamba na kuboresha miundombinu ya matibabu hivyo kupitia mfuko huu tutaweza kuongeza wataalamu,” amesema.

Rais Mwinyi amesema chuo hicho kimekuwa kikitekeleza majukumu yake ya kufundisha, kutafiti na kutoa huduma za afya na kwamba kimekuwa kikizalisha wataalamu mbalimbali wa afya.

“Kimekuwa chuo pekee nchini kinachofundisha wataalamu wa afya kwa ngazi zote na kina programu 20 za kibobezi ikiwemo upasuaji wa moyo, ubongo, figo na nyingine nyingi,” alisisitiza.

Amesisitiza kuwa uzalishaji wa wanataaluma umechangia kuanzishwa kwa vyuo vikuu na vya kati vya afya vinavyomilikiwa na watu binafsi ambavyo vimezalisha wataalamu wa afya.

Naye Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa matamanio ya Serikali ni kuhakikisha eneo la Mloganzila linakuwa mji wa taaluma za afya ifikapo mwaka 2050.

Amesema ujenzi wa Ndaki ya Tiba chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuongeza miundombinu ya kujifunzia na hosteli utakaokamilika Juni

Amesema lengo ni kuongeza wataalamu wa afya ndani na nje ya Tanzania wenye uwezo wa kupambana na changamoto mbalimbali za afya kutokana na maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya tabia nchi.

“Serikali inazidi kupambana na kupanua soko la ajira kuhakikisha wahitimu wetu wanaajiriwa punde wanapomaliza mafunzo yao. Tutakuwa na vituo vya umahiri hivyo kwa kufundisha vizuri, wahitimu wetu wanaweza kuajiriwa hapa au nje ya nchi,” amesema Mkenda

Amesisitiza kuwa chuo kitaendelea kusimamia miradi kwa uadilifu na weledi, kwa kuzingatia viwango vya ubora.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema wamekamilisha usajili wa Mfuko wa Maendeleo wa Ali Hassan Mwinyi (AHMMEF) kwa ajili ya kuanza kupokea fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo, wahitimu na watu binafsi.

Amesema kwa kushirikiana na familia wametengeneza katiba, sera na kanuni ili kuanza kupokea fedha.

“Mfuko huu ni kwa ajili ya kutoa msaada wa kifedha wa kudumu kwa miradi bunifu, programu za kitaaluma na ustawi wa wanafunzi na wanataaluma kuhakikisha kuwa MUHAS inaendelea kuwa chuo bora cha elimu ya afya na sayansi shirikishi, utoaji huduma za afya na utafiti nchini Tanzania,” amesema.
 

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi  akizungumza jambo katika Kongamano maalum la kumuenzi Mkuu wa Kwanza wa Chuo cha MUHAS na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi lililofanyika katika Kampasi ya Mloganzila leo Februari 28, 2025 jijini Dar es Salaam.

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza katika Kongamano maalum la kumuenzi Mkuu wa Kwanza wa Chuo MUHAS na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi lililofanyika katika Kampasi ya Mloganzila leo Februari 28, 2025 jijini Dar es Salaam.

 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa akizungumza katika Kongamano maalum la kumuenzi Mkuu wa Kwanza wa Chuo cha MUHAS na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi lililofanyika katika Kampasi ya Mloganzila leo Februari 28, 2025 jijini Dar es Salaam.

Related Posts