OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YASHIRIKI MKUTANO WA MAJADILIANO YA KIMKAKATI WA NGAZI ZA JUU 2025

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imeshiriki katika Mkutano maalumu wa Majadiliano ya Kimkakati ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050. Mkutano huo umefanyika tarehe 28 Februari, 2025 Jijini Dodoma.

Mkutano huo uliwahusisha Mawaziri kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini.

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa Mkutano uliofanyika mwaka 2024 ambapo pamoja na mambo mengine mkutano ulijikita zaidi katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi na namna ya kuweza kukabiliana nayo.

“Katika mkutano huu tumejadili masuala mbalimbali kuhusu Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi hususani kipindi hiki ambacho uchumi wa dunia hautabiriki”. Amesema Dkt. Mwigulu

Akizungumza mara baada ya Mkutano huo, Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius J. Njole ambaye alimwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kikao hicho, amesema kuwa katika mkutano huo wameweza kujadili masuala mbalimbali ya namna ya kuimarisha uhusiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Washirika wa Maendeleo.

“Tumeweza kujadili na kuona ni namna gani kama nchi inaweza kuendelea kunufaika na misaada mbalimbali au na mashirikiano baina ya Serikali na Washirika na Maendeleo”.
Amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria

Aidha, Mwandishi Mkuu wa Sheria ameeleza kuwa majadiliano hayo pia yameangazia namna nchi inaenda kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050 ambayo iko kwenye maandalizi, ambapo utekelezaji wa Dira hiyo unategemea misingi na mifumo ya kisheria hivyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina nafasi kubwa katika kuifikia Dira ya Taifa ya 2050.

“Utekelezaji wa Vision 2050 kwa kiasi kikubwa unategemea mifumo mbalimbali ya kisheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatarajia kuwa kiungo kikubwa katika utekelezaji wa jambo hilo”. Ameeleza Mwandishi Mkuu wa Sheria

Sambasamba na hilo, Bw. Njole amesema kuwa mkutano vilevile umejadili na kuyaangalia maeneo ya Siasa, Demokrasia na kukuza uwekezaji ambapo masuala hayo yataanza kutekelezwa na Washirika wa Maendeleo.





Related Posts