SIMBA imebakiwa na dakika 180 za kibabe katika mbio za ubingwa msimu huu, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu David akisisitiza anataka kwanza kumaliza mechi mbili zijazo kabla ya kujipanga kwe zilizosalia ili kuona wanatoboaje mbele ya Yanga.
Simba iliyopo nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 51 baada ya mechi 20 itaanza dakika 90 za kwanza kesho dhidi ya Coastal Union kisha kujiandaa kwa nyingine ijayo ya Dabi ya Kariakoo.
Hesabu za Fadlu zilifeli katika mchezo uliopita dhidi ya Azam baada ya kutoka na sare 2-2, huku ikivuna pointi moja tu iliyoifanya Simba kusalia nafasi hiyo ya pili.
Sasa Simba imebakiwa na kibarua kigumu ambacho wanatakiwa kukitimiza ndani ya siku nane tu, kitakachoanza kesho kabla ya kukabiliana na Yanga siku ya Wanawake Duniani (Machi 8).
Rekodi za duru la kwanza hazimpi usingizi kocha Fadlu, kwani katika mchezo wa kwanza dhidi ya Coastal Union ilipotoka sare 2-2, huku Yanga ikipoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti Fadlu amesema, Simba itakuwa na mtihani mgumu kwani inakwenda kucheza mechi ambazo hawakufanya vizuri mzunguko wa kwanza.
Amesema, kama watapoteza mechi hizo basi itakuwa imejiweka kwenye hatari kubwa ya kupoteza ubingwa, kwani watakuwa wamepoteza alama nyingi.
“Mechi kubwa zilizopo mbele yetu ni hizi za sasa dhidi ya Yanga na Coastal, hizi zingine tumeshamalizana nazo, lakini napata wakati mgumu kutokana na rekodi za mzunguko wa kwanza,” amesema Fadlu aliyetua msimu huu akitokea Raja Casablanca ya Morocco alikotwaa nao ubingwa msimu uliopita.
“Kwa sasa akili zipo katika mbio za Ubingwa kwani bado ziko wazi na mwanga unaonekana ila tukifanya makosa mechi mbili zijazo nuru itazima kabisa,” amesema Fadlu na kuongeza;
“Hizi kwetu ni mechi zinazobeba ajenda ya ubingwa na hatutacheka nazo kabisa, kwani tunahitaji alama sita za nguvu zitakazo tuweka katika nafasi nzuri ya Ubingwa. Moja kati ya mipango mikubwa niliyonayo ndani ya siku chache zilizosalia ni kutokuangusha alama ili tusiwe kwenye hatari.”