Simba yaifuata Coastal Union bila Camara, Che Malone

Simba itawakosa wachezaji wake Moussa Camara na Che Malone Fondoh katika mchezo wake wa Ligi Kuu kesho Jumamosi, Februari 28, 2025 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Wachezaji hao walipata majeraha hayo katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo dhidi ya Azam, Che Malone aliumia goti na kulazimika kutolewa katika kipindi cha kwanza ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Chamou Karaboue katika kipindi cha kwanza cha mchezo.

Kipa Moussa Camara alimaliza dakik zote 90 za mechi lakini wakati mchezo unaendelea alipata maumivu yaliyoonekana kuwa ya nyama za paja ambayo yalimshawishi refa Ahmed Arajiga kuita daktari wa Simba kumfanyia matibabu.

Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amethibitisha kuwa wachezaji hao wawili hawatokuwa sehemu ya kikosi cha Simba katika mchezo dhidi ya Coastal Union kwa vile wanaendelea kupata matibabu ya majeraha yanayowakabili.

“Che Malone Fondoh alipata majeraha akashindwa kuendelea na mchezo pamoja naye Mousa Pinpin Camara alimaliza mchezo lakini hakuwa sawasawa sana. Wote wamefanyiwa vipimo na tunasubiri majibu.

“Kwa hiyo taarifa rasmi ya kinachoendelea kwa upande wa afya wa Che Malone tutakuja kuwajuza punde tu mara baada ya kupata taarifa kutoka hospitalini.

“Wengine wote waliosalia wako vizuri, hakuna yeyote ambaye ana changamoto na wamerejea katika uwanja wa mazoezi,” amesema Ally.

Kukosekana kwa wachezaji hao muhimu wa safu ya ulinzi ya Simba dhidi ya Coastal Union kunatokea siku saba kabla ya timu hiyo kucheza mechi ngumu na yenye nafasi kubwa ya kuamua mbio za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Yanga, Machi 8 mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Camara amekuwa tegemeo la Simba langoni na kabla ya Coastal Union amecheza mechi zote za Ligi Kuu za timu hiyo akiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane huku akiongoza kwa kucheza idadi kubwa ya mechi za ligi bila kufungwa bao akifanya hivyo mara 15.

Related Posts