MABINGWA wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), Simba Queens imepangwa kuvaana na JKT Queens katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Samia Women Super Cup itakayochezwa jijini hapa, huku watani wao wa jadi, Yanga Princess ikipewa Fountain Gate Princess.
Michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza itapigwa kwa muda wa siku taty kuanzia Machi 4-7 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Fainali itapigwa na michuano hiyo na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu zitapigwa Machi 6 huku zawadi kwa washindi ikitazamiwa kutolewa Machi 8 ikiwa ni Kilele cha Siku ya Wanawake Duniani.
Akichezesha droo ya michuano hiyo, Meneja wa Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Baraka Kizuguto amesema anaamini ushindani utakuwa mkubwa kutokana na ubora wa timu shiriki.
“Bado tunawasiliana na watu wa Arusha kujua ni muda gani sahii wa kuanza kwa mechi make mechi mbili zitachezwa siku moja,” amesema Kizuguto na kuongeza;
“Kule kuna mechi za Ligi Kuu Bara zinaanza hadi saa 10:15 jioni hivyo tutaona ratiba imekaaje lakini kwa ratiba iliyopo sasa mechi hizi zitachezwa saa 8:00 mchana na saa 10:00 jioni.”
Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Arusha (ARWFA), Frida Minja amesema kwao ni furaha kuona mashindano makubwa kama hayo yanachezwa katika Mkoa wao.
Amesema timu zote zinazoshiriki ndio zile timu kubwa ambazo zinaleta ushindani katika Ligi Kuu ya Wanawake hivyo anaamini wadau wa soka Arusha watapata burudani.