Tabora United mwendo mdundo | Mwanaspoti

BAO la kujifunga la dakika ya 36 lililowekwa kimiani na beki Dissan Galiwango wa Dodoma Jiji katika harakati za kuokoa krosi na Nelson Munganga wa Tabora United, imeiwezesha nyuki wa Tabora kuvuna pointi tatu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Bao hilo lililoifanya Tabora kufikisha pointi 37 na kuendelea kung’ang’ania nafasi ya tano lilipatikana dakika ya 36 wakati Munganga kupiga krosi tamu iliyomlenga Offen Chikola aliyeruka hewani na kuukosa na kugongwa na kifua na beki huyo wa kati Mganda na kutinga wavuni.

Kujifunga kwa beki huyo kunamfanya aingie katika orodha ya waliojiwekwa akiwa mchezaji wa 12 hadi sasa katika Ligi Kuu, huku Dodoma ikiwa vinara kwa sasa kwa kujifunnga mara tatu ikiziacha Azam FC na KMC ilizokuwa ikilingana nao kila moja ikifunga mara mbili.

Kipigo hicho cha ugenini kimeifanya Dodoma Jiji kusalia katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 26 baada ya mechi 21, wakati Tabora ikiganda nafasi ya tano ikiwa na pointi 37 na kulipa kisasi kwani katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jamhuri, Dodoma Tabora ilifumuliwa mabao 2-0.

Kipa Daniel Mgore wa Dodoma ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kujifunga wakati wakilala bao 1-0 mbele ya Mashujaa, kisha akafuata beki Dickson Mhilu aliyejiweka walipovaana na Azam, ambayo katika mchezo huo nao iljikweka kupitia beki Yannick Bangala ambaye kwa sasa hayupo na timu hiyo baada ya kusajiliwa AS Vita ya DR Congo. Kipa Mohamed Mustafa ni mchezaji wa pili wa Azam kujifunga akifanya hivyo dhidi ya Tabora United iliyowafumua 2-1 mjini Tabora.

Waliojifunga kwa upande wa KMC ni Fredy Tangalo dhidi ya Azam na kipa Wilbol Maseke walipolala mbele ya JKT kwa mabao 2-0.

Wengine waliojifunga na beki wa Simba, Kelvin Kijili dhidi ya Yanga na kupoteza Dabi ya Kariakoo ya Oktoba 19 mwaka jana, yupo pia Jackson Shiga wa Fountain Gate wakati timu hiyo ikilala 5-0 mbele ya Yanga, Ladack Chasambi wa Simba aliyejifunga katika sare ya 1-1 na Fountain Gate.

Beki wa Coastal Union, Lameck Lawi alikuwa mchezaji wa tisa kujifunga mbele ya JKT Tanzanuia, beki Emmanuel Chigozie wa Tabora Utd naye alijiweka katika sare ya 1-1 dhidi ya TZ Prisons.

Related Posts