Mabalozi wa Serikali za Tanzania na Msumbiji wamefanya kikao cha ujirani mwema kilicholenga kudumisha uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Kikao hicho kimefanyika Leo Februari 27,2025 katika mkoani Mtwara kikiangalia namna ya kuimarisha vikao vya ujirani mwema kwa nchi hizo mbili na kudumisha uhusiano pamoja na kukuza uchumi kwa mkoa na wananchi kwa ujumla.
Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji phaustine Kasike amesema licha ya nchi hizo kuwa na ushirikiano mkubwa wa kihistoria hasa kwenye upande wa siasa na kijamii na kueleza kuwa upande wa kiuchumi bado haujafikia kiwango cha kuridhisha hivyo kupitia mikutano ya ujirani mwema itakuwa fursa ya kuwezesha nchi ya Tanzania kutangaza fursa zake za uchumi ambazo ziko katika maeneo ya kilimo,viwanda,utalii na biashara yatakayosaidia kupata masoko.
Naye Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania Ricardo Ambroisio, amesema manufaa ya kikao hicho ni kuona namna ya majimbo mawili kati ya Cabo Delgado na Mtwara yanaweza kunufaika nayo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala ameyaomba mataifa hayo mawili kupitia mabalozi wake kuendeleza ujirani mwema katika nyanja mbalimbali ambapo nyanja ya kiuchumi kiwe kipaumbele.
Aidha ameweka wazi hatua ya mataifa hayo mawili ambayo tayari jitihada za kuunganisha mawasiliano baina ya watu wake zimeanza kuchukuliwa katika mipaka yake na tayari wamesharekebisha kivuko cha MV Kilambo.