TCDC YAUNGA MKONO JITIHADA ZA SERIKALI KATIKA KUTANGAZA UTALII NCHINI

Kaimu Naibu Mrajis – Uhamasishaji, Consolata Kiluma, amesema kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) inaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kutangaza utalii nchini kupitia ‘Royal Tour’.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara ya Maafisa Ushirika katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire leo tarehe 28 Februari 2025.

Kiluma amesema ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Tume kuhakikisha Maafisa Ushirika wanaimarika katika utendaji kazi baada ya kupata mafunzo ya usimamizi wa vyama vya ushirika kwa maafisa Ushirika kutoka Kanda ya Kaskazini.

“Baada ya mafunzo haya, Tume iliona ni vyema kuwawezesha maafisa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ili waweze kujionea vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini. Hii siyo tu njia ya kuhamasisha utalii wa ndani, bali pia kusaidia kuboresha afya ya akili ya watumishi wetu, jambo linaloongeza ufanisi wanaporejea kwenye vituo vyao vya kazi,” alisema Kiluma.

Aidha, alibainisha kuwa Tume itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuandaa ziara kama hizi katika hifadhi nyingine nchini, ili Maafisa Ushirika waweze kufahamu zaidi kuhusu rasilimali za taifa na kushiriki kikamilifu katika kuvitangaza vivutio vya utalii.

Kwa upande wake, Afisa Ushirika wa Mkoa wa Arusha, Neema Neman, ameishukuru Tume kwa kuona umuhimu wa kuwapeleka kwenye hifadhi hiyo, akisema kuwa ziara hiyo imewasaidia kupumzika, kujifunza na kupata ari mpya ya kufanikisha majukumu yao ya usimamizi wa vyama vya ushirika.

Naye Mhifadhi wa Kitengo cha Utalii katika Hifadhi ya Taifa Tarangire, David Benedict, ameeleza kufurahishwa na ziara hiyo na kupongeza uamuzi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuhamasisha watumishi wake kutembelea hifadhi.

“Kupumzisha akili ni jambo muhimu baada ya kazi. Tunakaribisha wageni wengine kutoka Tume ili waone na kufurahia uzuri wa vivutio vyetu vya asili,” amesema Benedict.

Related Posts