TFF yaufungiwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeufungia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora hadi pale utakapofanyiwa marekebisho na kukidhi vigezo vya kutumika kwa mechi za ligi.

Uamuzi huo umetangazwa leo Ijumaa, Februari 28, 2025 muda mfupi baada ya mechi baina ya wenyeji Tabora United ambao wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji.

Taarifa iliyotolewa na TFF imefafanua kuwa uwanja huo haukidhi vigezo vya kikanuni.

“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeufungia uanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora kutumika kwa michezo ya Ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

“Miundombinu ya uwanja huo haikidhi matakwa ya Kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu.

Kufuatia uamuzi huo, timu zinazotumia uwanja huo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia uwanja mwingine kama Kanuni inavyoelekeza mpaka uwanja wao utakapofunguliwa,

baada ya kufanyiwa marekebisho na kukaguliwa na TFF.

“TFF inazikumbusha Klabu zote kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja,” imefafanua taarifa hiyo ya TFF.

Katika mchezo huo wa Tabora United dhidi ya Dodoma Jiji FC, nyasi za Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi zilionekana kukauka kwenye maeneo mengi ya uwanja na kuupa muonekano usiovutia.

Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi umekuwa ngome imara ya Tabora United kwani idadi kubwa ya pointi zake msimu huu imechukulia hapo.

Timu hiyo imecheza mechi 11 za Ligi ikiwa hapo ambapo imepata ushindi mara tano, imetoka sare nne na imepoteza michezo miwili.

Related Posts