Dar es Salaam. Madaktari bingwa wa watoto nchini wamependekeza itengenezwe aplikesheni maalumu itakayotumika kwenye simu janja kuwasaidia wataalamu wa afya kubaini na kutibu magonjwa adimu nchini.
Magonjwa adimu ni yale yanayowasibu watu wachache duniani, idadi yake ikikadiriwa kuwa kati ya 7,000 mpaka 8,000 ambayo huwakumba watu milioni 300 duniani, wengi wao wakiwa watoto chini ya miaka mitano.
Asilimia 88 ya madaktari waliohojiwa katika utafiti ulioangazia changamoto zinazowakabili madaktari wa watoto nchini, wamesema lipo tatizo kubwa katika ugunduzi wa magonjwa hayo.

Utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), umeonyesha asilimia 88 ya madaktari wamewahi kuona mtoto mwenye ugonjwa adimu, asilimia 94 wametibu mtoto hao au dalili zake na kushindwa kujua anasumbuliwa na nini, huku asilimia 60 wameyatibu maradhi hayo miezi michache iliyopita.
Akisoma matokeo ya utafiti wa madaktari wa watoto kuhusu magonjwa hayo leo Ijumaa, Februari 28, 2025, Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto, Mariam Noorani amesema utafiti ulibaini upungufu mkubwa kwenye elimu, mafunzo na utaalamu wa magonjwa adimu.
“Asilimia 82 ya madaktari wamependekeza kuwe na aplikesheni maalumu yenye maelekezo kamili, itakayotumika kwenye simu janja, kuwasaidia wataalamu wa afya kubaini na kutibu, ili kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa adimu,” amesema.
Amesema utafiti huo uliofanywa kwa madaktari bingwa wa watoto 168 waliojaza dodoso.

“Changamoto kubwa, wote walisema wanapata changamoto ya kutoweza kufanya vipimo vinavyohitajika na asilimia 70 wamesema walishindwa kupata tiba huku asilimia 40 wakishindwa kupata tiba shirikishi,” amesema Dk Noorani.
Awali akizindua mkutano huo, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi amewataka watafiti kulifanyia kazi zaidi eneo hilo.
“Wanasayansi tufanye machapisho yenye manufaa na majibu ya changamoto kwenye jamii na tuache kufanya tafiti za kupata vyeo pekee. Kuna magonjwa mengi chanzo chake ni lishe, upungufu wa vitamini E, B au Calcium,” amesema Profesa Janabi.
Katika upande wa uchunguzi na matibabu ya magonjwa adimu, Daktari bingwa wa magonjwa hayo, Kandi Muze kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili amesema:
“Tanzania bado hatuna takwimu za magonjwa adimu ni magonjwa gani, watoto wangapi wanaathiriwa na matibabu wanayoyapata ni yapi.”
Dk Muze amesema wagonjwa wengi hukaa muda mrefu hospitali na hakuna namna za kutibu haya magonjwa kwenye nchi nyingi zinazoendelea na magonjwa mengi yanasababishwa na vinasaba.
“Asilimia 95 ya magonjwa haya hayana tiba ya moja kwa moja. Kwa Tanzania Muhimbili watoto 192 tuliwafanyia utafiti na hawa wanagunduliwa wanapozaliwa mpaka miaka mitano,” amesema.
Miongoni mwa magonjwa hayo, anataja gaucher unaosababishwa na kukusanyika kwa mafuta baada ya mtoto kukosa kimeng’enyo cha mafuta na hivyo kuhitaji kimeng’enyo bandia.

“Mtoto atahitaji dawa za sindano ambazo atachoma kila baada ya wiki mbili kwa maisha yake yote. Ugonjwa mwingine unaitwa galactosemia huu unasababishwa na maziwa ya mama na mama akiacha kumnyonyesha mtoto anapona,” amesema Dk Muze.
Hali hiyo inathibitishwa na binti anayetibiwa ugonjwa adimu kwa Sh10.4 milioni kila mwezi.
Sindano moja anayotakiwa kuchomwa kila baada ya wiki mbili, inagharimu Dola 2,000 za Marekani, sawa na Sh5.2 milioni za Tanzania.
Yusra Kaundu (13), ni mtoto aliyezaliwa na ugonjwa gaucher unaosababisha kimeng’enyo cha mafuta mwilini kushindwa kufanya kazi na hivyo kongosho kuvimba.
Yusra anayesoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Msumi aligundulika kuwa na tatizo hilo baada ya vipimo vyake kupelekwa Afrika Kusini.
Baba wa Yusra, Hamis Kaundu (42) amesema yeye na mke wake walihangaika kwa muda mrefu bila mafanikio.
Kufuatia hilo, wataalamu wamependekeza iwepo sera ya vipimo vya vinasaba nchini na huduma hizo zipatikane kwa bei nafuu.
Mtaalamu wa magonjwa ya vinasaba hapa nchini, Dk Siana Nkya amesema kati ya magonjwa 8,000 adimu, asilimia 70 husababishwa na hitilafu katika mpangilio wa vinasaba.