Vikundi 60 vyalamba mkopo Sh1.13 bilioni Ilemela, vyaonywa ‘kuponda maisha’

Mwanza. Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imetoa mkopo wa Sh1.13 bilioni kwa vikundi 60, huku Serikali ikionya dhidi ya matumizi yasiyofaa ya fedha hizo.

Hafla ya kukabidhi mkopo huo imefanyika leo Ijumaa, Februari 28, 2025, chini ya mpango wa asilimia 10 ya makusanyo ya halmashauri, ambapo wanawake wanapewa asilimia nne, vijana asilimia nne na makundi maalumu asilimia mbili.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ummy Wayayu amesema kati ya vikundi 60 vilivyonufaika, vikundi vya wanawake ni 39, vijana 17 na makundi maalumu manne.

Katika mchakato wa uombaji, ofisi yake ilipokea maombi kutoka kwa vikundi 148, ambapo wanawake walikuwa 113, vijana 28 na makundi maalumu saba.

Baada ya uhakiki, vikundi 80 havikukidhi vigezo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa katiba na ofisi inayotambulika.

Wayayu amesema vikundi 39 vya wanawake vitapokea Sh618 milioni, vikundi 17 vya vijana Sh492 milioni na vikundi vinne vya makundi maalum Sh24 milioni.

Ameongeza kuwa vikundi 32 vilivyokidhi vigezo vitapatiwa mkopo katika awamu inayofuata.

Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo, Renatus Mulunga amewataka wanufaika wa mkopo huo kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuepuka matumizi yasiyo sahihi.

“Mlikuwa mkituliza kuhusu lini mtapata mkopo huu, sasa msitafute visingizio vya kushindwa kuurejesha. Mtakapoponda mali, mtashindwa kufanya marejesho,” ameonya Mulunga.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mariam Msengi amewahimiza wanufaika wa mkopo huo kushirikiana na wataalamu watakaofuatilia matumizi ya fedha hizo badala ya kufunga ofisi na kukwepa ukaguzi.

Kwa upande wake, Yohana Matahe, aliyepokea mkopo kwa niaba ya kundi maalumu, ameishukuru Serikali kwa fursa hiyo na kuahidi kuutumia kuboresha maisha yake na familia yake.

Jackson Taranga, mwakilishi wa vikundi vya vijana kutoka kikundi cha Dira Photo Group, ameahidi kuutumia mkopo huo kwa tija na kuurejesha kwa wakati.

Naye Spezia Alex ameiomba Serikali kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kusaidia vikundi hivyo kutumia fedha hizo kwa manufaa na kuzitatua changamoto zinazojitokeza katika shughuli za uzalishaji.

Related Posts