Yanga yaendeleza dozi, yaifyatua Pamba Jiji

YANGA imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi za Ligi Kuu Bara baada ya leo jioni kutoa kichapo cha mabao 3-0 ugenini mbele ya Pamba Jiji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Katika mchezo huo wa raundi ya 22, Yanga imepata ushindi kupitia kwa wachezaji wa kigeni, la kwanza likifungwa dakika ya 28 na beki wa kushoto, Chadrack Boka kwa mpira wa friikikii nje kidogo ya eneo la 18 uliojaa moja kwa moja nyavuni ukimuacha kipa Yona Amosi akiruka bila mafanikio.

Mabao mengine mawili yamefungwa na staa wa timu hiyo, Stephane Aziz Ki dakika ya 75 na 77 na kumfanya afikishe jumla ya mabao saba kwa sasa katika Ligi Kuu, huku Maxi Nzengeli aliyeasisti moja ya mabao hayo akifikisha asisti ya sita msimu huu.

Aziz Ki ametua dakika tatu kufunga mabao hayo mawili, akiwa ameingia uwanjani dakika 46 baada ya kuanzia benchi kipindi cha kwanza akichukua nafasi ya kiungo Khalid Aucho.

Ushindi huo wa 19 unaendelea kuihakikishia Yanga nafasi ya kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi 58 baada ya michezo 22, huku ikiongeza gepu la pointi dhidi ya watani, Simba wenye alama 51 na kwenda kwenye mchezo wa dabi ya Kariakoo wakiwa na matumaini makubwa.

Huo ni ushindi wa tano kwa Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi aliyetua Jangwani Februari 4, mwaka huu akichukua mikoba ya Saed Ramovic, ambapo ameiongoza katika michezo sita dhidi ya Ken Gold (6-1), Mashujaa (5-0), JKT Tanzania (0-0), Singida Black Stars (2-1) na KMC (6-1).

Kwa upande wa Pamba Jiji, kichapo hicho kinaiacha katika nafasi ya 12 na alama zake 22, huku kikiwa ni kipigo cha saba kwa Pamba Jiji chini ya Fredy Felix ‘Minziro’ aliyetua klabuni hapo Oktoba 17, 2024 akiiongoza katika michezo 15, kushinda tano na sare tatu.

Kipindi cha kwanza kilianza taratibu kwa mashambulizi ya kushtukiza na pande zote zikisomana zaidi, huku Pamba wakionekana kuwa hatari zaidi kwa dakika 20 za mwanzo na kutengeneza mashambulizi mengi yaliyolenga lango la Yanga na kumfikia kipa, Djigui Diarra na kama ingeongeza umakini zaidi ingeweza kuambulia chochote.

Pamba imefanya mashambulizi hayo dakika dakika ya nne kupitia kwa winga, Zabona Mayombya ambaye aliichekecha safu ya ulinzi ya Yanga na kupiga shuti ambalo limeishia mikononi mwa kipa, Djigui Diarra.

Dakika ya sita, Pamba Jiji imefanya jaribio lingine kupitia kwa kiungo mshambuliaji, Abdoulaye Camara ambaye amewachmbua mabeki wa Yanga na kupiga shuti lililotoka nje kidogo ya lango.

Winga, Zabona Mayombya ambaye alikuwa tishio zaidi kwa safu ya ulinzi ya Yanga katika dakika 20 za kwanza, alifanya jaribio lingine la kuzitafutia timu yake bao katika dakika ya 17 lakini shuti lake likadakwa na kipa.

Winga huyo aliendelea kuisumbua Yanga ambapo dakika ya 22 alitengeneza shambulizi lingine baada ya Khalid Aucho kupoteza mpira lakini akapiga shuti ambalo lilikwenda nje ya lango.

Yanga walirejea mchezoni na kuanza kuukamata mchezo Dakika ya 25 ambapo walitengeneza shambulizi kupitia krosi ya Maxi Nzengeli ikamkuta Israel Mwenda akaitenga kwa Duke Abuya lakini shuti lake likapaa juu ya lango.

Dakika ya 28, Boka aliifungia Yanga bao la kuongoza kwa mkwaju wa friikikii baada ya Mudathir Yahya kuangushwa na mabeki wa Pamba Jiji.

Baada ya bao hilo, Yanga iliamka zaidi na kuendelea kulisaka lango la Pamba Jiji ambapo dakika ya 30 Mudathir alipiga shuti kali nje ya 18 ambalo lilipaa juu kidogo ya lango.

Dakika ya 34, manusura Pamba iandike bao la kusawazisha baada ya beki wa Yanga, Ibrahim Bacca kuanguka na kupoteza mpira ulionaswa na straika wa Pamba, Mathew Tegis aliyebaki peke yake na Bakari Mwamnyeto na kupiga shuti ambalo lilipanguliwa na Djigui Diarra na kuwa kona.

Dakika ya 44 manusura Yanga wapate bao la pili katika shambulizi lililotokana na kona iliyochongwa na Maxi Nzengeli na kusababisha piga nikupige shuti la Mzize likagonga mwamba, kisha Mudathir Yahya akapiga tena lakini kipa akaokoa na kuondoa hatari hiyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko ya wachezaji ikimtoa kiungo Khalid Aucho na kuingia Stephan Aziz Ki dakika ya 46, huku Jonathan Ikangalombo akiingia dakika ya 69 kuchukua nafasi ya Clement Mzize na kuongeza mashambulizi katika lango la Pamba Jiji.

Dakika ya 82 Yanga iliwatoa Prince Dube na Maxi Nzengeli huku nafasi zao zikichukuliwa na Clatous Chama na Kennedy Musonda, pia alitoka Mudathir Yahya na kuingia Abubakar Salum (Sure Boy).

Pamba Jiji nayo ilifanya mabadiliko dakika ya 66 ikiwapunzisha Deus Kaseke na Abdoulaye Camara na kuwaingiza Habib Kyombo na John Nakibinge ili kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji.

Katika kuhakikisha anakwenda kwenye mchezo wa dabi ya Kariakoo Machi 8, mwaka huu dhidi ya mtani, Simba akiwa na kikosi kilichokamilika, Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi alipumzisha baadhi ya wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza huku wengine wakianzia kwenye benchi.

Katika mchezo huo, nyota Aziz Ki, Dickson Job walianzia benchi, huku Pacome Zouzoua akikosekana kabisa, ambapo kiungo Khalid Aucho alipumzishwa kipindi cha pili baada ya mapumziko hakurudi na nafasi yake ikachukuliwa na Aziz Ki, jambo ambalo lilionekana ni kama kocha huyo alichukua tahadhari ya kuwaepusha wachezaji wake muhimu wasipate majeraha katika mchezo huo.

IKANGALOMBO AKIWASHA DK 21

Baada ya kutoonekana katika kikosi cha Yanga tangu aliposajiliwa dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu, beki wa pembeni, Jonathan Ikangalombo raia wa DR Congo hatimaye jana alikiwasha katika mchezo wake wa kwanza Ligi Kuu Bara akiwa na uzi wa Wananchi.

Ikangalombo ambaye amezua maswali mengi kwa mashabiki wa timu hiyo kutokana na kutoonekana kwake katika kikosi cha Yanga, alianzia katika benchi kwenye mchezo huo dhidi ya Pamba Jiji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mmwaga maji huyo huyo aliingia dakika ya 69 akichukua nafasi ya mshambuliaji, Clement Mzize na kuandika historia ya mchezo wake wa kwanza wa ligi kuwa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kuwa fiti kwa winga huyo huyo anayesifika kuwa na kasi na mbio kumeongeza matumaini zaidi katika kikosi cha Yanga ambacho mchezo ujao kitachuana na watani wao, Simba katika dabi ya Kariakoo Machi 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Related Posts