Dar es Salaam. “Naumia kuona jitihada tulizofanya kwa miaka mingi za ukombozi wa mwanamke zinarudishwa nyuma na watu wanaotaka kuendeleza mfumo dume, kwa kujaribu kuaminisha umma kwamba kumuinua mtoto wa kike kunamshusha au kumdumaza mtoto wa kiume.
“Mjadala huu unatengenezwa na watu wanaoamini katika mfumo dume na hawataki kwa namna moja au nyingine kuona ukombozi wa mwanamke, hili limeibuka zaidi baada ya kupata Rais mwanamke, kuna ambao bado hawaamini kwamba mwanamke anaweza kuwa kiongozi.”
Hii ni kauli ya Profesa Ruth Meena, mwanaharakati wa haki za wanawake, katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.
Profesa Meena ni miongoni mwa wanawake takribani 17,000 kutoka mataifa mbalimbali walioshiriki mkutano wa Beijing, nchini China mwaka 1995 ulioweka misingi ya kupambania ajenda ya ukombozi wa mwanamke.
Anasema kwa kipindi cha miaka 30 hatua mbalimbali zimepigwa katika kumkomboa mwanamke, ikiwemo kufungua milango kwa watoto wa kike kupata elimu na kuiwa Serikali imeondoa ada ili kuruhusu watoto wote, hata wale wa familia maskini, kupata elimu.
Anasema uamuzi wa kuruhusu kurejea shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ujauzito, ni fursa kwa wasichana wengi kutimiza ndoto zao hata baada ya kukabiliwa na changamoto zilizowafanya waangukie kupata ujauzito.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kati ya mwaka 2014/2015 na 2020/2021 Tanzania imeongeza asilimia 9.5 ya wanafunzi wanaoandikishwa shule za msingi na asilimia 14.3 katika elimu ya sekondari.
Takwimu hizo zinaonyesha pia asilimia 59 ya wanawake wote nchini wamepata fursa ya kupata elimu ya msingi, wanaume wakiwa asilimia 63.7; huku wanawake asilimia 2.2 wamepata elimu ya ufundi ukilinganisha na wanaume asilimia 3.8.
Takwimu hizo zinaonyesha wanawake waliopata elimu ya chuo kikuu ni asilimia 0.8 ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 1.9.
Profesa Meena anasema mwanga wa mafanikio ukianza kuchomoza, mfumo dume unataka kurudi kwa kasi kutokana na uwepo wa watu wachache wanaoona jitihada zinazofanyika kumkomboa mtoto wa kike zinalenga kumdumaza mtoto wa kiume.
Hali hii ya ubaguzi huathiri makuzi ya mtoto wa kike, hasa kufikia au kunufaika na rasilimali kama ardhi na huduma za msingi za kijamii. Pia haki ya kufikia na kunufaika na matokeo ya elimu, huduma za afya na uhuru wa kusikilizwa.
Profesa Meena ambaye kitaaluma ni mbobezi wa sayansi ya siasa, aliyeshiriki kuandika machapisho mbalimbaali kuhusu usawa wa kijinsia, anasema kwa kiasi kikubwa mjadala huo unaendelezwa na wanasiasa na kuambukiza wanajamii wenye fikra hasi kuhusu ukombozi wa mwanamke.
Anasema mjadala huo unakuja wakati ambapo bado mwanamke anakabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo za ukatili wa kingono, ndoa za lazima, vipigo au hata kukutana na vikwazo kadhaa anapopambana kujikwamua kiuchumi.
“Ni mjadala unaondelezwa na watu wachache wanaoogopa mabadiliko katika ngazi zote, ni wale ambao hawaamini wangetawaliwa na Rais mwanamke, wale ambao wanafikiri majimbo ni mali zao, wanafikiri ndoa ni uhusiano wa kiutawala badala ya mapenzi.
“Ndio hao wanaotaka kuaminisha umma kwamba ndoa zinapovunjika basi ni kwa sababu mwanamke wa sasa ameelimika, anajitambua na anaweza kusema hapana kwa aina zote za ukandamizaji,” anasema na kuongeza:
“Hizi ni fikra potofu, ukombozi wa mwanamke una dhamira ya kujenga misingi ya usawa wa jinsia kwa wanawake na wanaume au watoto wa kike na wa kiume, siyo kutaka upande mmoja utawale upande mwingine.”
Kauli ya Profesa Meena inashabihiana na aliyoitoa hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya programu ya mwanamke kiongozi inayotolewa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).
Akitoa mfano, Rais Samia alisema alipoingia madarakani kulikuwa na mishale mingi iliyoelekezwa dhidi yake kutokana na watu kukosa Imani, kwamba mwanamke anaweza kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
“Wakati ule hakukuwa na watu waliokuwa wanaamini kwamba kuna mwanamke anaweza kufika hapa, kuna waliothubutu kusema tuna Rais wa kuambiwa fanya na atafanya tu, kuna waliothubutu kusema hatuna Rais tuna ‘house girl’, kuna waliothubutu kusema maamuzi ya ‘kitchen party’ wakiwa na maana yale niliyokuwa nafanya.
“Hiyo ndiyo ilivyokuwa imani ya wenzetu anaposimama mwanamke, lakini leo nadhani wote wamebadilika, kwa hiyo unapotaka kuondoa na kujenga imani kwa wenye mtazamo mwingine basi fanya yale yanayotarajiwa,” alisema Rais Samia aliyeingia madarakani Machi, 20s21.
“Tumefanya yaliyotarajiwa ndiyo maana yale mawazo kwa kiasi kikubwa yameondoka, yule ‘house girl’ hayupo tena, maamuzi ya ‘kitchen party’ hayapo tena yamekuwa ya maana sasa, kwa hiyo tambueni tuna jukumu la kuelimisha jamii kufahamu kwamba usawa wa kijinsia si mapambano ya wanawake kutaka kuwa juu ya wanaume,” alisema.
Profesa Meena anasema kama Dira ya Taifa inavyoelekeza kwamba tunataka Taifa lililoelimika, jitihada za ukombozi wa mtoto wa kike hazipaswi kubezwa, badala yake nguvu kubwa inapaswa kuongezwa kwa kundi hilo kwa sababu bado liko nyuma.
“Dira inataka tuwe na Taifa lililoelimika kwa maana watoto wote bila kujali jinsia zao wapate elimu na washiriki kutumia talanta zao katika maeneo mbalimbali. Ukifanya utafiti wa kisayansi kuangalia data, utaona bado wanawake wanakutana na changamoto lukuki hata kwenye hizo harakati za kujikwamua kiuchumi.
“Kila kitu kinapimwa na takwimu, sisi tunaofanya hizi harakati tunaona bado mtoto wa kike yupo nyuma na anaendelea kukumbana na aina mbalimbali za unyanyasaji, ikiwemo vipigo na wakati mwingine kunyimwa haki ya kupata elimu,” anasema.
Akitoa mfano wa maisha yake, Profesa Meena anasema alikulia katika familia yenye mfumo dume, baba yake hakuwa tayari kumsomesha lakini baada ya miaka mingi baba huyo alikiri kuwa huo ulikuwa ujinga wa wazee wa zamani hivyo anashangaa kuona vijana wa sasa bado hawaoni umuhimu wa kusomesha mtoto wa kike.
“Elimu ndiyo msingi wa ukombozi, tunapaswa kusimama kikamilifu kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu na isionekane kusoma kwake kunaweza kuwa kikwazo kwenye jamii.
“Hata mimi kusoma kwangu hakukuwa rahisi, nimekulia kwenye mifumo ya ukandamizi. Baba hakutaka kusomesha watoto wa kike lakini niling’ang’ania na bahati nzuri kaka yangu mmoja alikuwa upande wangu, alijitoa kuhakikisha napata elimu. Hata ilipofika wakati aliposhindwa kunilipia ada, nilikwenda kwenye baraza la kijiji kuomba msaada, nilijielezea kwenye baraza na kufanikiwa kuwashawishi wajumbe nikasoma bure,” anasema.
Anasema fursa ya kupata elimu alihakikisha anaitumia vyema na tangu hapo alijiona ana wajibu wa kupambana kwa ajili ya ukombozi wa wanawake, msingi mkubwa ukiwa elimu.
Profesa Meena anasema kama ambavyo yeye alivyobahatika kusoma katikati ya mfumo kandamizi anaamini hata sasa wanaweza kuwapo wanajamii ndani ya mfumo huo ambao wanaweza kuleta mabadiliko na kuhakikisha suala la usawa wa kijinsia linakuwa ajenda endelevu na yenye nguvu.
“Tangu wakati huo harakati zimekuwa ndani ya nafsi yangu, naupinga mfumo kandamizi, sitaki kuona hilo linafanyika kwa mtoto wa kike wala wa kiume, lakini kwa vile kwenye uwiano mtoto wa kike anaumia zaidi, ndiyo maana tunaweka nguvu zaidi kulitetea kundi hilo.
“Hivyo basi, huu uoga wa wachache usiturudishe nyuma tunaotetea haki za wanawake na watoto wa kike kuendelea kupaza sauti. Wote tuna jukumu la kufanya ili kuhakikisha uwepo wa dunia ambayo wanawake na wasichana wote wawe huru, kusiwe na ukatili katika kizazi hiki kwa kujenga mifumo imara zaidi ya uwajibikaji na inayofikia watu wengi,” amesema.
Profesa Ruth Meena alizaliwa Moshi, mkoani Kilimanjaro mwaka 1946. Ni mwanaharakati wa haki za binadamu, mtetezi wa haki za wanawake, mtaalamu na mwandishi wa machapisho kadhaa kuhusu jinsia na uwezeshaji wa wanawake.
Alikuwa profesa wa kwanza mwanamke wa Kitanzania katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Alifanya kazi kwa miaka 27 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1980 – 2007 na miaka tisa katika vyuo vya ualimu na shule za sekondari (1971 – 1980).
Amefanya kazi kama mshauri katika mashirika mbalimbali ya haki za wanawake yakiwamo TGNP Mtandao na Women Fund Tanzania Trust (WFT).
Pia ni mwanachama wa majukwaa mbalimbali yakiwamo ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia, uongozi wa wanawake na katiba.