Trump, Rais wa Ukraine walivyocharukiana White House

Washington. Mazungunzo kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na Volorymyr Zelensky yameishia njiani baada ya kushindwa kuelewana kuhusu hatima ya vita ya Russia dhidi ya Ukraine.

Ilianza kama utani wakati wa kikao hicho ambacho kimehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance na waandishi wa habari.

Kila upande ulianza kuelezea kile ambacho wamejadiliana kuhusiana na makubaliano yaliyokuwa yanatarajiwa kutiwa saini. Awali Trump alieleza kuwa makubaliano hayo ni pamoja na kusaini  mkataba unaoiruhusu Marekani kuchimba madini adimu (rare minerals) katika ardhi ya Ukraine.

Wakati mrejesho wa hatua iliyofikiwa kuhusu makubaliano hayo ya mkataba wa madini mambo yalikuwa sawa ila yakaanza kwenda mrama pale Trump alipohamisha mada na kuingia suala la kupata mwafaka wa mzozo kati ya Ukraine na Russia ya Vladimir Putin.

Trump kwenye suala hilo alienda moja kwa moja na kumtaka Rais Zelensky, kuingia makubaliano na Russia ya kumaliza vita hivyo, la sivyo Marekani itajindoa katika mazungumzo hayo na haitoendelea kuifadhili tena wala kuipatia misaada Ukraine.

Wawili hao walikatizana mara kwa mara wakati wa majibizano yao kwa namna isiyo ya kawaida ndani ya White House.

Wakati fulani, Trump, alionekana mwenye hasira, alimwambia Zelensky kuwa hana shukurani ya kutosha kwa msaada wa kijeshi na kisiasa kutoka Marekani na kwamba alikuwa ‘anacheza kamari’ na vita vya Tatu vya Dunia.

Kwa upande wake, Zelensky alimjibu Trump bila kificho kuwa hapaswi kuwa na “maafikiano yoyote” na Rais wa Russia, Vladimir Putin lakini Trump alisisitiza kuwa  ni lazima kufanya makubaliano ili kupata amani dhidi ya hasimu wake Russia.

Mkutano huo ulipangwa kutanguliwa na kutiliana  saini makubaliano ya madini, jambo ambalo halikutokea.

Baada ya Trump kuonekana kama anakabwa kooni kwa hoja na Zelenskyy,  Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance akaingilia kati na kuanza kumkaripia Zelensky hadharani, mazungumzo yalianza kwa Vance kumwambia Zelensky kwamba vita vilipaswa kumalizika kwa njia ya kidiplomasia.

Zelensky aliuliza, “Diplomasia ya aina gani?” kabla ya kushutumiwa na makamu wa Rais, Vance aliyemuita Zelenskyy kuwa ‘ana dharau.

Rais wa Ukraine, Volorymyr Zelensky akiaga wakatiki akiondoka White House jana Februari 28, 2025.

Majadiliano yalizidi kuwa makali, huku Trump na Vance wakimlaumu Zelensky kwa kutokuwa na shukurani kwenye misaada ambayo Marekani imekuwa ukiipatia Ukraine kwa zaidi ya miaka mitatu ya vita na Russia.

Trump amesema Zelensky hakuwa na haki ya kuwaambia Wamarekani jinsi wanavyopaswa kujisikia kuhusu amani na mzozo huo unaoendelea huko, badala yake alipaswa kusikiliza na kutii anachoelekezwa.

Baada ya majibizano hayo, muda ukapita kisha Rais Zelensky alionekana akiondoka Ikulu ya White House kwa kutumia gari yake.

Baada ya Zelensky kuonekana amekerwa na kuondoka, Trump aliingia Truth Social, ambao ni mtandao wake wa kijamii na kuandika: “Zelensky ameidharau Marekani katika Ofisi ya Oval yenye heshima kubwa.”

“Tulikuwa na mkutano muhimu sana leo White House,” aliandika. “Kuna mambo mengi yaliyofahamika ambayo yasingeweza kueleweka bila mazungumzo yenye moto na shinikizo.”

“Cha kushangaza ni kuona kinachotokea kutokana na hisia na nimegundua kuwa Rais Zelensky hayuko tayari kwa amani ikiwa Marekani itahusika, kwa sababu anaamini usaidizi wetu unampa nguvu kubwa kwenye mazungumzo. Sitaki faida, nataka amani.” ameandika.

Ameongeza kuwa Zelensky “anaweza kurudi atakapokuwa tayari kwa amani”.

Miongoni mwa mambo ambayo hasimu wa Zelensky, Vladimir Putin ambaye ni Rais wa Russia anayataka yatimizwe ndiyo asitishe mapigano na taifa hilo ni pamoja na Ukraine kukubaliana na ukweli kwamba maeneo ambayo yametwaliwa ni mali halali ya Russia.

Maeneo hayo ni mikoa ya Donetsk, Luhansk, Zaporizhia, Kherson, Pokrovisk, na Crimea ambayo imetwaliwa tangu mwaka 2014. Hata hivyo, msimamo wa Zelensky ni kwamba anataka Russia iyarejeshe mikononi mwake na kuondoa wanajeshi wake katika ardhi hiyo.

Suala lingine ni kwamba Russia inaitaka Ukraine kufuta wazo lake la kutaka kujiunga Jukuiya ya Kujilinda ya Nato, kwa kile ambacho Putin anadai kuwa kufanya hivyo ni kuhatarisha usalama wa Russia na mipaka yake.

Hata hivyo, Zelensky amekuwa akifanya ziara za kila mara kwenye majukwaa na mikutano ya jumuiya ya Ulaya (EU) kuomba apewe uanachama ili aanze kunufaika na faida zake ambazo ni pamoja na kuimarishiwa ulinzi.

Suala la tatu, Rais Putin anamtaka Zelensky aitishe uchaguzi utakaomweka madarakani kihalali kwa kile anachodai Rais huyo yupo madarakani kwa Sheria ya Kijeshi (Martila Law), hivyo atakubali kuingia kwenye meza ya mazungumzo iwapo raia wa Ukraine watamchagua kwa kura halali.

Hata hivyo, suala hilo, lilipingwa vikali hata na bunge la Ukraine ambapo wawakilishi na wajumbe wa bunge hilo walipiga kura na kumpitisha Zelensky kuwa Rais halali wa taifa hilo. Katiba ya Ukraine inaruhusu wabunge kutamka hadharani iwapo wanamtambua kuwa ni Rais wa taifa hilo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari

Related Posts