Makomandoo Yanga waizuia Simba kufanya mazoezi kwa Mkapa usiku

Mashabiki wa Yanga maarufu kwa jina la makomandoo wameuzuia msafara wa watani wao, Simba kuingia Uwanja wa Benjamin Mkapa, usiku huu.

Simba imefika uwanjani hapo kwa lengo la kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo huo, lakini dakika chache kabla ya saa 1:00, walitimuliwa na makomandoo hao.

Kwa mujibu wa kanuni ya 45 ya uendeshaji wa Ligi Kuu toleo la 2024, timu mgeni wa mchezo inaruhusiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja ambao utatumika kuchezwa mchezo husika kwa muda ambao mechi hiyo itaanza na hivyo Simba ilikuwa sahihi kufika kwa ajili ya mazoezi yao.


MWANZO MWISHO JINSI YANGA WALIVYOIZUIA SIMBA KUINGIA KWA MKAPA USIKU HUU, DAH KILICHOTOKEA …

Hata hivyo, Simba ikakutana na tukio hilo uwanjani hapo, baada ya makomandoo hao kuzuia msafara huo nje ya geti wakidai hakuna utaratibu huo kwenye mchezo baina ya timu hizo.

“Wao walikuwa wenyeji wa mchezo uliopita mbona hawakuruhusu sisi kuja kufanya mazoezi na tuliitikia katazo lao na kama hawaamini hili basi lao litaingia uwanjani bila vioo,” walisikika makamandoo hao ambao ni maalum kwa kazi za ulinzi wa timu hiyo.

Ilipofika saa 3:10 usiku makomandoo hao wakaliamsha zogo wakitaka basi la Simba kuondoka uwanjani hapo kwa kuwa muda wa kufanya mazoezi umeshapita, hatua ambayo iliwalazimu makocha wa wekundu hao na baadhi ya viongozi wao kufanya kikao kifupi nje ya geti Kuu la kuingia uwanjani hapo.

Baada ya kikao hicho kilichotumia dakika tatu tu, Kocha wa Simba Fadlu Davids na wasaidizi wake walirejea ndani ya basi kwa lengo kwenda hadi geti kuu la kuingia uwanjani.

Hata hivyo, makomandoo hao  hawakukubali na kwenda kukaa mbele ya basi hilo na kuwaaambia ligeuze kisha basi hilo kutii amri na kugeuka kisha kuondoka uwanjani hapo.

Endelea kufuatilia tovuti na mitandao ya kijamii ya Mwanaspoti kujua zaidi undani wa sakata hilo.

Related Posts