Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya maendeleo kwa watanzania ikiwemo ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Ametaja miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere, lakini daraja la kigongo Busisi huku akieleza mafanikio hayo ni silaha ya ushindi kwa Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi wa Oktoba 2025.
Hayo amesema ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutembelea wilaya za mkoa wa Dar es Salaam aliyoanza Machi 4 Jijini hapo kuongea na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuanzia ngazi ya Shina hadi Wilaya kuhamasisha wajitokeze kwenye shughuli ya kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpigakura litakaloanza Machi 17 hadi 23, 2025 kwa mkoa huo.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa PTA Sabasaba Temeke, Makalla amesema jitihada alizozifanya anapaswa kupongezwa kwakuwa ameweka historia ya maendeleo nchini.
“Hapa Dar es Salaam kila mahali panachimbuliwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mabasi ya mwendokasi, ndiyo maana bandari zinaboreshwa, reli za kisasa zinajengwa ni kutokana na usimamizi mzuri,” amesema Makalla nakuongeza
“Chini ya Rais Samia uchumi unakua na uwekezaji unakua juzi nilipita kituo cha uwekezaji kilitaja miradi mbalimbali inayoonyesha kukua kwa uwekezaji Tanzania mafanikio yote hayo yanatokana na maono ya Rais Samia katika utawala wake,” amesema.
Kulingana na maelezo ya Makalla katika mkutano huo amesema maendeleo na mafanikio yaliyofanywa chini ya usimamizi wa Rais Samia yatakuwa chachu ya kuvuna ushindi wa kimbunga katika uchaguzi Mkuu mwaka huu 2025.
“Kikubwa jitokezeni kwenye kuboresha taarifa zenu kwenye daftari la kudumu la mpigakura, kwani mafanikio yaliyopatikana ni silaha kubwa ya ushindi kuelekea katika chaguzi mkuu,” amesema
Mbali na hayo, ametoa ahadi kwa watanzania kuweka wagombea wanaokubalika na wananchi kwenye nafasi ya udiwani na Ubunge katika uchaguzi Mkuu unotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Pia ameahidi kuja na ilani itakayokuja kujibu kilio na changamoto wanazopitia wananchi na kuongeza hata kampeni zitakazofanywa na chama hicho katika kuuza wagombea wake zitakuwa zinafanyika kwa kuzingatia mfumo wa 4R zilizoasisiwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Rais Samia Suluhu Hassan.