Simba waikalia kikao Yanga usiku, Ahmed Ally afunguka haya

Uongozi wa Simba umeitisha kikao cha dharura usiku huu kujadili kuzuiliwa kwa timu yao kufanya mazoezi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam leo.

Simba ilienda uwanjani hapo saa 1:00 usiku ili ikifika muda ambao mchezo huo utachezwa waanze kufanya mazoezini, lakini ilizuiwa na wanaosemekana kuwa makomandoo wa Yanga na hivyo kulazimika kuondoka.

Habari za uhakika zimefichua, baada ya tukio hilo, Simba wameitisha kikao na muda mfupi ujao watatoa taarifa rasmi ya kile walichokiamua.

“Tunakutana na kuna uamuzi mzito na mgumu ambao tunaweza kuuchukua ili iwe fundisho kwa mamlaka za soka juu ya kuheshimu kanuni,” kimesema chanzo cha uhakika kutoka Simba.

Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally amesema watatoa taarifa rasmi.

“Wakubwa wanajadiliana na punde watatoa tamko,” amesema Ahmed Ally.

Kwa mujibu wa kanuni ya 45 ya uendeshaji wa Ligi Kuu toleo la 2024, timu mgeni wa mchezo inaruhusiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja ambao utatumika kuchezwa mchezo husika kwa muda ambao mechi husika itaanza.

Related Posts