UVCCM Mwanza yaungana na walimu wasio na ajira, yaishauri Serikali

Mwanza. Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Mwanza umesema unaunga mkono harakati za Umoja wa Walimu Wasio na Ajira (Neto) huku ukiitaka Serikali kuchukua hatua za kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana.

Februari 21, 2025 umoja huo wa walimu wasio na ajira ulifanya mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ukidai kutoridhishwa na mchakato wa ajira ya ualimu, ukidai wasomi wa kada hiyo waliokosa ajira tangu mwaka 2015 hadi 2023.

Umoja huo umekuwa ukiishinikiza Serikali kuangalia suala hilo kwani wahitimu wengi wapo mitaani hawana ajira huku baadhi zikiwa na upungufu.

Tayari Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akizungumza Machi 3, 2025 na wakuu wa taasisi na mashirika jijini Dodoma alisema amepanga kukutana na vijana hao ili kuwasikiliza.

Waziri Simbachawene alisema atakutana na vijana hao Jumatatu Machi 10, 2025 yeye na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili kuwasikiliza.

Katikati ya vuguvugu hilo, leo Ijumaa Machi 7, 2025, Mwenyekiti wa UVCCM Mwanza, Seth Masalu amekutana na waandishi wa habari kuzungumzia suala hilo, akisema kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita amekuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa vijana wa mkoa huo wakitaka awasaidie.

“Kuna kundi la vijana wanajiita Neto. Sisi kama vijana wa Mkoa wa Mwanza tuliwasikiliza vizuri na tunaunga mkono harakati zao, tunaunga mkono mawazo yao kama vijana wana haki ya kupigania masilahi yao katika nchi yao,” amesema Seth.

Hata hivyo, Kada huyo wa CCM amesema changamoto ya ajira siyo ya walimu peke yao, bali ni changamoto ya vijana wa kada tofauti tofauti wanaomaliza vyuo vikuu na vya kati.

“Ninalo ombi kwa Serikali lakini vile vile naomba niishauri Serikali…kwa kuwa Simbachawene aliahidi kukutana na vijana hao (Neto) umoja wa UVCCM Mkoa wa Mwanza unamshauri kikao atakachokutana nao kiwe chakujenga ili watakapotoka hapo wawe na suluhisho ya changamoto zao,” amesema.

“Lakini nyuma nilishasikia vilevile Naibu Waziri wa Tamisemi anasema wataoa nafasi kwa wakurugenzi ikiwezekana waweze kuajiri ajira za mikataba, ninatamani kuona mawazo hayo yawe maelekezo ili wakurugenzi wapambane na changamoto hii na si tu iwe kwa matakwa yao, bali Serikali ielekeze kwamba halmashauri zote  nchini pale wanapoona makusanyo yao ni mazuri basi waweke malengo ya kuajiri vijana ili kupunguza changamoto hii,” amesema.

Pia ameiomba Serikali ifanye tathimini katika mashirika ya umma yanayo legalega sababu ya kutokuwa na watumishi wa kutosha iyaelekeze yaajiri vijana hata kwa ajira za mikataba ili kupunguza changamoto hiyo.

“Najua Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa alisema kwamba Serikali haiwezi kuajiri watu wote kama ambavyo haiwezi kuajiri waandishi wa habari wote, kama ambavyo haiwezi kuajiri wataalamu wa afya wote ni kweli lakini ninaimani kuna hatua ambazo zikichukuliwa zinaweza kwenda kupunguza changamoto hii kwa kiasi fulani,” amesema.

Amesema uwepo wa vijana wengi mitaani ambao hawana ajira kuna weza kuwa na madhara kama vile Serikali kupata hasara, ongezeko la vijana kujiingiza kwenye uhalifu wa wizi, vijana kuwa tegemezi kwa Serikali lakini pia hatari ya kupoteza wapiga kura kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

“Ukifuatilia rekodi za TCU (Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania) kwa mwaka zaidi ya vijana 50,000 wanahitimu vyuo vikuu..sasa fikiria tunavyoongea sasa wanahudumia wanafunzi karibu 70,000 kwa kila mwaka wa masomo wanafunzi wanaojiunga vyuo vikuu,” amesema.

Amesema wanaamini Serikali itatoka haraka hadharani na kuja na majibu ya kukabiliana na hali ya changamoto ya ajira kwa vijana ili kuokoa taifa, uchumi na vijana wenyewe.

“Sisi ni Chama cha Mapinduzi, huu ni mwaka wa uchaguzi hawa vijana ni wapiga kura tunawategemea waje watupigie kura watuchague kwa hiyo kuna haja ya haraka Serikali kulifanyia kazi suala hili ili kurudisha imani kwa chama,” amesema.

Aidha, amewataka vijana kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwenye halmashauri nchini, ili kujipatia kipato kupitia shughuli za ujasiriamali wakati wakisubiri ajira za serikalini.

Related Posts