Unguja. Baadhi ya vyama vya siasa vimesema vinaridhishwa na shughuli ya uandikishaji wa daftari la mpigakura kutokana na utulivu unaoendelea tofauti na kipindi cha nyuma.
Wakizungumza katika vituo vya uandikishaji Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi Machi 7, 2025, viongozi na mawakala wa vyama hivyo, wamesema uzoefu unaonyesha kipindi cha nyuma katika nyakati kama hizo kilikuwa kinaibuka fujo na vurugu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir amewapongeza wananchi kwa kudumisha amani na kuepusha migongano isiyo ya lazima.
“Wananchi wanajitokeza kila mwenye haki anapata haki yake,” amesema.
Ameir amewahamasisha wananchi ambao bado hawajajiandikisha kujitokeza kupata haki yao kwani daftari hilo ni la mwisho na mtu ambaye hatokuwemo katika daftari la kudumu la wapigakura, hatoweza kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Chama cha UPDP, Hamad Mohammed Ibrahim, amesema wanaridhika namna kazi hiyo inavyoendeshwa.
Amesema mawakala wa vyama vyote wanaridhika na hakuna mwananchi mwenye sifa ambaye hapati haki yake ya kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapigakura.
Wakala wa ACT Wazalendo katika Kituo cha Uandikishaji cha Kwerekwe, Mcha Kheir Ali, licha ya kukiri kutokuwapo kwa changamoto za mivutano, amesema kuna changamoto ya wananchi kutojitokeza kuchukua vitambulisho vyao.
Amesema bado ipo kazi kwa vyama vya siasa kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kwenda kuchukua vitambulisho vyao vya kupigia kura.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jaji Joseph George Kazi amesema katika kuzungukia maeneo ya uandikishaji, wamebaini hali ya utulivu na hakuna anayenyimwa haki yake kujiandikisha.
Amesema katika wilaya hiyo wanatarajia kuandikisha wapigakura wapya 13,759 kutokana na makadirio ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Amewataka wenye sifa kuendelea kujitokeza kujiandikisha ili wapate haki yao ya kupiga kura.
Amani Ayoub Makame, Sheha wa Shehia ya Kwerekwe na Mwanahawa Haji Juma, Sheha wa Shehia ya Mwembemajogoo wamesema zipo changamoto ndogondogo za wananchi kutofuata taratibu za uhamiaji lakini zinashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu.
“Wapo wanaotaka kuandikishwa kwa kitambulisho cha Mtanzania jambo ambalo sio sawa,” amesema Sheha wa Shehia ya Kinuni, Ramadhan Khamis Mahonge.