Arusha. Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Isack Amani amewataka wanawake na wasichana nchini kujiheshimu, kujiamini na kusimama imara katika maadili wakijiepusha na vitendo vya kujidhalilisha kwa namna yoyote ile.
Ametaka maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake (IWD) leo Machi 8, 2025 itumike kuzalisha mawazo chanya kuhusu wanawake na wasichana.
Askofu huyo ameyasema hayo leo Jumamosi Machi 8, 2025 katika maadhimisho hayo ambayo kitaifa yanafanyika Arusha ambapo mgeni rasmi ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema ukatili na kudhalilishana siyo sahihi, ni lazima yazalishwe mawazo chanya kuwawezesha wanawake kujiamini.
“Siku hii inatufanya tujiulize tunamwelewa vipi Mwenyezi Mungu. Mungu ameelekeza vipi kuhusu wanawake?
“Tujiulize kama desturi na mila zetu zinaendana na mpango na malengo ya Mungu kuhusu tunavyopaswa kuelekeana. Tangu mwanzo Mungu aliweka mfanano, aliweka umoja, usaidizi, usawa, haki na uwezeshaji kati ya jinsia mbili, siyo jinsia tatu wala nne,” amesema.
Amesema jamii inatakiwa ithamini na kuendeleza jinsia zote, ndio maana mpangilio wa ndoa na familia kama atakavyo Mungu lakini leo hii kuna ambao wanaamua kujipatia watoto, hawataki ndoa hawataki familia, huo siyo mpango wa Mungu.
“Wanawake wakijitunza, wakawa safi, hakutakuwa na mashangazi. Ukatili na kudhalilishana hutoka katika dhana na fikra zisizoendana na mpango wa Mungu, leo maadhimisho yazalishe mawazo chanya kuhusu wanawake na wasichana.
“Wanawake wagombee nafasi za uongozi katika nyanja mbalimbali,” amesema Askofu Amani.
Endelea kufuatilia tovuti ya Mwananchi na mitandao yake ya kijamii kwa taarifa zaidi.