Dabi ya Kariakoo, mzani upo upande huu

MASHABIKI wa Yanga na Simba wanaendelea kusubiri kuona ni kitu gani kitatokea kabla ya timu hizo kushuka katika pambano la Ligi Kuu lkwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, leo.

Mchezo huo huenda ukatoa taswira ya vita ya ubingwa kutokana na pengo la pointi lililopo baina yao, japo Yanga inaingia ikiwa na rekodi nzuri baada ya mchezo kwanza kushinda bao 1-0 – la kujifunga la Kelvin Kijili Oktoba 19, 2024. 

Mchezo huu utakaokuwa wa 114 kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu 1965, unatarajiwa kuwa na ushindani kama kawaida wakati zinapokutana, ingawa rekodi zinaibeba zaidi Yanga tofauti na Simba.

DABI 01

Mchezo huo utakuwa wa 63 kwa miamba hiyo kukutana katika Ligi Kuu siku ya Jumamosi tangu 1965, ambapo kati ya 62 iliyopita, Yanga imeshinda 27, huku Simba ikishinda 16 wakati 19 ni sare.

Katika michezo hiyo Yanga ndio ambayo imekuwa mwenyeji mara nyingi zaidi (michezo 38) huku Simba ikiwa mara 24.

Kwenye michezo hiyo 62, yamefungwa mabao 128, ambapo Yanga imefunga 75, huku Simba ikifunga mabao 53.

Kichapo kikubwa kinachokumbukwa Jumamosi ni kile Yanga ilichoifunga Simba wakati ikifahamika Sunderland cha mabao 5-0, Juni 1, 1968 yaliyofungwa na Maulid Dilunga na Salehe Zimbwe mawili kila mmoja na Kitwana Manara.

Hata hivyo, Simba ndio timu ya kwanza kushinda mchezo uliopigwa Jumamosi wakati huo ikiitwa Sunderland ilipoifunga Yanga bao 1-0, Novemba 26, 1966 lililofungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Mustafa Choteka dakika ya 44, ya mechi hiyo.

DABI 02

Ukiachana na Yanga kuonekana kupata matokeo mazuri inapocheza na Simba siku ya Jumamosi, lakini asikwambie mtu bana! Kwani hata michezo iliyopigwa mwezi Machi rekodi zinaonyesha zinakibeba zaidi kikosi hicho cha mitaa ya Twiga na Jangwani.

Rekodi zinaonyesha pia timu hizo zimekutana mara 10 katika michezo ya Ligi Kuu iliyopigwa mwezi Machi tangu 1965, ambapo Yanga imeshinda minne na kutoka sare mitano, huku Simba ikiambulia ushindi mmoja kati ya hiyo.

Pia, Yanga ndio timu ya kwanza kushinda mchezo uliopigwa mwezi huo ukiwa ni wa nne kukutana tangu 1965 uliopigwa Machi 30, 1968 ilipoifunga Simba kipindi hicho ikiitwa Sunderland bao 1-0 la Kitwana Manara katika dakika ya 28.

DABI 04

Ushindi mwingine kwa Yanga ulikuwa wa bure wa mabao 2-0 Machi 3, 1969 baada ya Simba iliyokuwa inaitwa Sunderland kugoma kuingia uwanjani ikashinda pia (2-1) Machi 27, 1993 na ule wa bao 1-0 la Bernard Morrison Machi 8, 2020.

Michezo mitano ya sare ni ya (1-1), Machi 10, 1984, (1-1), Machi 15, 1986, (0-0), Machi 18, 1995, (0-0), Machi 26, 2006 na mchezo wa Machi 5, 2011, ulioisha kwa kufungana bao 1-1 na kuzua tafrani uwanjani kwa mwamuzi wa kati, Oden Mbaga.

Mchezo pekee Simba ilioshinda mwezi huo, ulikuwa wa Machi 8, 2015, ukiwa ni wa 94 kukutana katika Ligi Kuu Bara ambao kikosi hicho kilishinda bao 1-0 la nyota wa zamani, Mganda Emmanuel Okwi dakika ya 52.

DABI 03

Najua unajua, ila nikukumbushe tu mchezo baina yao una kumbukumbu na vituko vya kushtua kwa sababu Machi 3, 1969, Yanga ilipewa pointi za bure na ushindi wa mabao 2-0, baada ya Simba kipindi hicho ikiitwa Sunderland kugoma kuingia uwanjani.

Jambo lingine ambalo linakumbukwa baina ya timu hizi wakati zilipokutana mwezi huu, lilikuwa ni tukio la Machi 5, 2011, ambapo mwamuzi, Oden Mbaga alilikataa bao la kusawazisha la Simba, kisha akalikubali kwa kushirikiana na msaidizi wake.

Katika mchezo huo wa 86, kwa timu hizo kukutana, Yanga ilianza kupata bao la penalti ya Stefano Mwasyika dakika ya 59, kisha Simba ikasawazisha dakika ya 73, kupitia kwa aliyekuwa mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Mussa Hassan Mgosi.

Bao hilo la Mgosi, ndilo liliamsha tafrani baada ya mwamuzi, Oden Mbaga kulikataa kwa madai ya mshambuliaji huyo alikuwa tayari ameotea, ingawa alilikubali baada ya kupata msaada wa mwamuzi msaidizi namba moja, Maximillian Nkongolo wa Rukwa.

DABI 05

Simba ina kibarua kigumu cha kulipiza kisasi baada ya kuchapwa michezo yote mitatu mfululizo iliyopita ya Ligi Kuu Bara, ikianza na cha mabao 5-1, Novemba 5, 2023, (2-1), Aprili 20, 2024, kisha kile cha mwisho cha bao (1-0), Oktoba 19, 2024.

Mchezo huu ni wa kisasi zaidi kwa Simba kutokana na rekodi mbovu kwa wapinzani wao kwa sababu mara ya mwisho kushinda ilikuwa ushindi wa mabao 2-0, Aprili 16, 2023, yaliyofungwa na beki wa zamani wa timu hiyo, Henock Inonga na Kibu Denis.

Related Posts