Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa amewapa kibarua Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) kuhakikisha wanawaelimisha Watanzania kuhusu ajenda ‘No reform no election’ (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) inayolenga kushinikiza mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.
Dk Slaa amesema kibarua hicho kitahusu pia, Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) na Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), akisisitiza hakuna kupoteza muda bali kutekeleze jukumu hilo ili mageuzi yapatikane.
Mbunge huyo wa zamani wa Karatu mkoani Arusha ameeleza hayo, leo Jumamosi Machi 8,2025 katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na Bawacha na kufanyika Mlimani City.
“Bila kuchelewa Bawacha, Bavicha na Bazecha ndiyo wenye watu, imani yangu mkirudi kwenye vituo vyenu ndani ya siku tatu au nne mtakwenda kuwaelesha Watanzania kuhusu ‘No reform no election.’
” Watu wakielewa tufanikiwa, tusipotumia jeshi hili ( Bawacha) mikutano ya hadhara pekee hatutafanikiwa, tunahitaji kubuni mbinu mbalimbali Bazecha, Bavicha na Bawacha mkirudi nyumbani mkalifanyie kazi,” amesema Dk Slaa.

Amesema mabaraza hayo yasipotekeleza wajibu huo, basi ‘No reform no election,’ haitawezekana, lakini ana imani hilo hawatalishindwa.
Dk Slaa amesema kwa miaka 30 upinzani umekuwa ukidai haki na marekebisho ya Katiba, lakini jambo hilo halijafanikiwa, ndiyo maana anaunga na mkono hoja ya Chadema ya ‘No reform no election’ili haki itendeke katika chaguzi.
Kwa nyakati tofauti mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amekuwa akisema wamekuja ajenda hiyo ili kushinikiza mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi, akisema mifumo iliyopo hivi sasa siyo rafiki hasa kwa upinzani.