Dar es Salaam. Minyukano ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Kigamboni umeuibua uongozi wa chama hicho ukieleza kwamba haufurahishwi na vitendo hivyo, huku ukiahidi kuwashughulikia wahusika kama hawatajirekebisha.
Minyukano hiyo inatokea baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dk Faustine Ndugulie ambaye pia alikuwa mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, kufariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Dk Ndugulile alipeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kushinda baada ya kuvuka kiunzi cha kura za maoni zilizofanyika katika mchakato wa ndani, akipata kura 190 dhidi ya Paul Makonda aliyemfuatia kwa kura 122.
Akizungumzia vurugu hizo kwenye mkutano wa ndani wa CCM uliofanyika Wilaya ya Kigamboni, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema hawafurahishwi na makada wao kupigania Jimbo la Kigamboni huku akieleza kuwa imefikia hatua watuhumiwa wanashtakiana wenyewe kwa wenyewe.
Amesema pamoja na mbunge wa jimbo hilo (Dk Ndugulile) alifariki dunia, haina maana makada waendeleze vurugu, ni muhimu wanaohitaji wazingatie kanuni na sheria za chama hicho kwa kusubiri muda ufike.
“Jambo hili ni baya hata kama jimbo halina mbunge, hatuwezi kuvumilia vurugu zinazoendelea kufanyika huku Kigamboni, imefikia hatua viongozi mnafanya mikutano na kupita kuwatambulisha wagombea, mnajua kabisa mnavunja sheria,” amesema na kuongeza:
“Kigamboni hapa tumeondokewa na mbunge, basi kelele zimekuwa nyingi kama vile jimbo halina mtu wa kulalamika, mnakuwa hata hamna woga, mnajibebea wagombea kwa mabega yenu bila hata wasiwasi, hadi mnawapeleka kwenye mikutano ya hadhara kuwatambulisha, hiyo haikubaliki hata kidogo,” amesema.

Amewaonya kwamba wakiendelea na mtindo huo, “mtawafanya watu wenu hao wapotezea muda kwani tutawaengua kulingana na marekebisho ya kikatiba waliyofanya.
“Kigamboni nimeyasikia mengi, hamna hata haya, mikutano ya hadhara mmebeba wagombea eti mnamuona huyu, mkome muache! Mnakiharibia taswira nzuri chama chetu, mnaofanya hivi ni viongozi kabisa,” amesema.
Amesema haiwezekani viongozi wamepewa dhamana halafu wanaanza kuvunja kanuni wanazosimamia na kusema wanaendea kuomba bajeti za kuzunguka “Nawaambia mnataka kumfilisi huyo mtu”.
“Mtu huyo atapoteza kamati ya siasa fanyeni kazi kuchunguza yanayoendelea msidhani hatujui, tulieni kama riziki ipo ipo tu, kote nilikozunguka sijakemea kama hapa, tafsiri yake Kigamboni mmezidi,” amesema Makalla huku akipigiwa makofi na kushangiliwa na makada wa chama hicho.
Kwa mujibu wa Makalla, amesema imefikia hatua katika jimbo hilo kumeanzishwa msemo mpya “lishe kwanza afya baadaye” (pesa kwanza sera baadaye) na kusema hawafurahishwi.
“Mwenyekiti wa CCM Kigamboni, Sikunjema, msifikiri hatujui, tunafahamu, imefikia hatua watu wanaandaa vikao na kupita kutambulisha watu wakijua ni kosa. Sasa nakutaka udhibiti jambo hili, ukishindwa CCM mkoa fanyeni kazi yenu,” amesema Makalla.
Makalla amesema baadhi ya makada wameanza kuandika barua kuomba bajeti ya fedha kwa watu ili waandae vikao, kupita kuwaonyesha na kuwatambulisha huku akiwaonya wanaofanya mchezo huo wanawarahisishia kuwaengua kwenye mchujo.
“Inafikia hatua mtu anajua mwenyewe anafanya makosa halafu anakuja kumshtaki mwenzake bila kujua naye yupo katika makosa, viongozi jirekebisheni, sitaki kusikia. Kama mtu ameanza kutumia fedha sasa, hadi kufikia wakati wa uchaguzi itakuwaje?” amesema.
Katika mkutano huo uliotaaliwa na shangwe za makada wa chama hicho, Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Sikunjema alisimama na kuomba msamaha huku akiahidi kutekeleza maagizo hayo.
Wakizungumza na Mwananchi, makada wa CCM KIgamboni wamesema ziara aliyofanya kiongozi huyo itatuliza joto la kisiasa katika maeneo hayo kwa kile walichoeleza katika nafasi za udiwani na ubunge, mvutano ni mkubwa.
“Natokea Kata ya Tungi, anakotoka Meya wetu, lakini kuna watu kama saba wanataka nafasi ya udiwani na wanajipitisha kila uchwao. Kwa kuchimbwa mkwara huu, watu watatulia ingawa hawawezi kuacha,” amesema Rashid Mohammed.
Mkazi mwingine wa Kigamboni, Rhoda Richard ameshauri ziara hizo kufanyika mara kwa mara hasa katika kipindi hiki wanachoelekea kwenye kura za maoni, kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu.
Ziara ya Makalla Mkoa wa Dar es Salaam imehitimishwa Wilaya ya Kigamboni ambapo alijikita katika kuhamasisha viongozi wa chama hicho kutoka ngazi ya shina hadi wilaya kujitokeza kwa wingi kwenye shughuli ya kuboresha daftari la kudumu la mpigakura linalotarajiwa kuanza Machi 17 hadi 23, 2025.