LICHA ya kugubikwa na sintofahamu ya kuchezwa mwa mchezo wa Kariakoo Dabi kati ya wenyeji Yanga na Simba, mashabiki wa timu hizo wameendelea kujitokeza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ilipopangwa kuchezwa mechi hiyo.
Shabiki mmoja wa Simba aliyejulikana kwa jina la Elius amesema amesikitishwa na uamuzi uliochukuliwa na viongozi wa timu hiyo ya Msimbazi kugomea mchezo, huku akiitaka Bodi ya Ligi (TPLB) kuweka sheria kali ili kupunguza vitendo vya aina hii.
“Mimi nimetoka Kagera na nimekuja hapa Dar es Saalam tangu Jumanne, nimejichangachanga ili kufanikisha kuja, ila jambo la kusikitisha nimesikia taarifa za Simba kugomea mchezo huo, kiukweli ni mambo ya kihuni na Serikali iingilie kati suala hili,” amesema na kuongeza;
“Kitendo cha makomandoo wa Yanga walichokifanya kiukweli sio cha kiungwana kwa sababu Simba imetumia haki ya kimsingi, naiomba Bodi ya Ligi (TPLB), itumie kanuni ya kupokwa pointi ili iwe fundisho kuliko hiki kinachoendelea.”
Shabiki huyo amesema kitendo cha Simba na Yanga kupigwa faini ya Sh1 milioni hakijitoshelezi kwani kiasi hicho ni kidogo kwao na endapo wangekatwa pointi ingekuwa fundisho.
“Tangu nizaliwe nilikuwa sijawahi kuangalia dabi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, leo nimekuja kwa sababu naamini tutashinda mabao 3-0, na Elie Mpanzu atawasumbua sana wachezaji wa Yanga na hapo ndipo ningeamini safari ya ubingwa imewadia.”
Kupitia taarifa iliyotolewa jana na uongozi wa Simba, Wekundu wa Msimbazi wamesema hawatashiriki mchezo wa leo kwa kile walichokieleza kufanyiwa vitendo visivyokuwa vya kiungwana na makomandoo wa Yanga wakati walipowasili Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi kwa mujibu wa kanuni inavyoeleza.
Mchezo huo ambao umepangwa kuchezwa kuanzia saa 1:15 usiku, ni wa kisasi zaidi kwa Simba kwani mechi ya kwanza baina ya miamba hiyo iliyopigwa Oktoba 19, mwaka jana, Yanga ilishinda bao 1-0, la kujifunga la beki wa kulia, Kelvin Kijili akiwa katika harakati za kuokoa mpira, huku pia Wana Msimbazi wakiwa wametoka kupoteza mechi nne mfululizo dhidi ya timu hiyo ya Wananchi.