Dar es Salaam. Wanawake wa Chama cha Demokarsia na Maendeleo (Chadema), wamejumuika kusherehekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake.
Wanawake hao waliovalia sare za vitenge wametoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar na wamekusanyika leo Jumamosi Machi 8, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Shughuli hiyo imehudhuriwa na mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu pamoja na viongozi waandamizi wa chama hicho, akiwamo John Mnyika (katibu mkuu), John Heche (makamu mwenyekiti bara), Aman Golugwa (naibu katibu mkuu) na Ali Ibrahim (naibu katibu mkuu Zanzibar.

Maadhimisho hayo yalipangwa kuanza saa tatu asubuhi, yalianza kuchangamka mchana baada ya viongozi wakuu kuingia ukumbuni.
Ingawa aliyekuwa mwenyekiti, Freeman Mbowe hakuwepo ukumbi, lakini aliibua shangwe baada jina lake kutajwa na katibu mwenezi wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Siglada Mligo wakati akitoa salamu zake kwa dakika tano.
Wakati Katibu Mkuu wa Bawacha, Pamela Massay akitoa utambulisho wa meza kuu na wageni waalikwa ndipo akaambiwa kuwa walioko meza kuwa wapewe kipaumbele cha kuzungumza lolote, alianza Mhazini wa baraza hilo, Joyce Mukya kisha akafuata Mligo.

Katika maelezo, Mligo aliwashukuru viongozi wakuu waliopita akiwamo Mbowe akisema ana mchango mkubwa katika chama hicho kikuu cha upinzani.
“Mheshimiwa mwenyekiti nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipomtambua mwenyekiti wetu wa zamani Freeman Mbowe. Baba yetu ndiye aliyetupa jeuri na ukuu huu,” amesema Mligo ndipo ukumbi ukalipuka kwa shangwe na washiriki wakanyuka kwenye viti kuelekea meza kuu kumpongeza.
” Mheshimiwa mwenyekiti (Lissu) Bawacha tutaongoza gurudumu la mabadiliko, hii vita sote tunahitajiana. Baba yangu mwamba (Mbowe) endelee kumpumzika umefanya mengi hata Lissu anatambua hilo,” amesema Mligo.

Katibu mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa naye aliibua shangwe baada ya kutambulishwa kama mgeni mwalikwa katika tukio hilo.
Baada ya jina lake kutajwa, ukumbi uliripuka kwa furaha, Dk Slaa alilazimika kusimama mara mbili ikiwa ni ishara ya upendo kwa kina mama hao waliokuwa wakimshangilia kwa kupiga makofi.
Akiwaribisha wanawake hao, Mwenyekiti wa Bawacha Kanda ya Pwani, Rose Moshi amesema baraza hilo litakuwa mstari wa mbele kusukuma ajenda ya mabadiliko sambamba na kusimamia ajenda ya bila mabadiliko, hakuna uchaguzi.