Unguja. Wakati Zanzibar ikianza rasmi usajili wa uwekezaji katika hatifungani inayofuata misingi ya Kiislamu (Zanzibar Sukuk), jumla ya miradi 12 yenye thamani ya Sh1.115 trilioni inatarajiwa kutekelezwa kupitia fedha za uwekezaji huo.
Kati ya miradi hiyo, mitatu ipo chini ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, saba ipo chini ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na wizara Afya na Maji, Nishati na Madini zikiwa na mradi mmoja mmoja kila wizara.
Akiwasilisha taarifa hiyo wakati wa kuzindua usajili wa uwekezaji huo leo Machi 8, 2025 Mwenyekiti Mtendaji Yusra Sukuk Co Ltd ambao ndio washauri elekezi, Sheikh Mohamed Issa amesema hatifungani hiyo iliyozinduliwa Februari 22, 2025 ilikuwa haijaanza kusajili hivyo dirisha la kwanza limezinduliwa leo linatarajiwa kufungwa Aprili 6 mwaka huu.
“Mtaona hii ni miradi mikubwa na ya kimkakati na itakapomalizika inaandikwa kuwa ni miradi iliyotekelezwa na Sukuk ili kila mmoja aone fedha zake zimefadhili kitu gani,” amesema.
Miradi hiyo ni pamoja na masoko ya samaki katika kiwanda cha Kama, Fungu refu, Mkoani huku kwenye afya utajenga Hospitali ya Binguni na kusimamia upotevu wa umeme.
“Katika barabara zitakazojengwa kupitia Sukuk ni Machomanne Wawi hadi Vitongoji kilomita saba, Chwaka, Kilindi hadi sokoni kilomita 23, Kizimbani hadi Kiboje, Unguja Ukuu, Uzi Ng’ambwa na Kitogani.
Barabara nyingine ni Mkwajuni Matemwe, Mkwajuni hadi Kijini na Kizimkazi hadi Makunduchi ambapo zote zitagharimu Sh498.4 bilioni.
Katika mradi mwingine ambao unatarajiwa kutekelezwa kupitia mpango huo ni bandari ya Mangapwani ambayo itatumia Sh399.8 bilioni ujenzi wa uwanja wa ndege Terminal 2 utagharimu Sh62.4 bilioni.
Amesema kutokana na uwekezaji huo zitahitajika Sh159 bilioni kuwalipa wawekezaji watakaowekeza kwenye Sukuk.
Ametaja miongoni mwa faida za kuwekeza katika hatifungani hiyo ni pamoja na kupunguza msongo wa mawazo kwa sababu hakuna riba, hivyo mtu hatofikiria kulipa madeni
“Hakuna makato yoyote ya kodi, hakuna hasara, unachangia maendeleo na uwekezaji huu unalinda imani za watu,” amesema.
Katika uzinduzi huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema baada ya kumaliza hatua hizo ni kutoa uelewa kwa wadau tofauti.
Amesema tayari kuna viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi nao wameshawekeza kwenye Sukuk huku kukiwa na watendaji wengine serikalini ambao wameshaanza.
Mkurugenzi wa Zanzibar Sovereignty Sukuk, Dk Masoud Rashid Mohamed amesema hiyo ni kampuni ya Serikali ambayo imewekwa kisheria kwa ajili ya kukusanya fedha za utekelezaji wa miradi ya miundombinu na kukuza uchumi.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, nishati na Madini, Joseph Kilangi amesema ipo haja kutengeneza dirisha la mfanyakazi wa Serikali kuchukua fedha zake katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) kuwekeza kwenye hatifungani hiyo.
Pia amesema ipo haja kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji wengi kutoka nje wapate fursa hiyo.
Akijibu hoja hizo, Waziri Saada amesema mfumo wa hatifungani hiyo unaruhusu mtu mmojammoja kuwekeza kwa hiyo ni vyema watumishi kutumia fursa hiyo badala ya kutegemea fedha zinazowekwa ZSSF kwani kule kuna dirisha maalumu kwa ajili ya mfuko huo.
“Hii ni hatifungani nzuri kwa sababu kiwango cha kwanza kinaanzia Sh1 milioni hivyo mnaweza kuunda kikundi na kuwekeza kwa pamoja, amesema Dk Saada