Dar/Mikoani. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Mkoa wa Dar es Salaam, Mwajabu Mbwambo amewataka wanawake watambue katika uchaguzi wa mwaka 2025 wana jukumu la kuandika historia mpya ya kuwapo wengi katika nafasi za uamuzi.
Akizungumza kwenye mkutano wa ndani wa CCM wilayani Kigamboni uliohudhuriwa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, leo Machi 8, 2025 amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, wanawake idadi yao ni kubwa ikilinganishwa na wanaume hivyo kigezo hicho kinatosha kuibuka vinara na kuandika historia iwapo watajipanga.
“Tupo mwaka wa uchaguzi katika nafasi ya urais hakuna mpinzani, mgombea ni Mwenyekiti wetu wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, lakini katika nafasi nyingine za udiwani na ubunge tuzichangamkie lakini siku zote adui wa mwanamke ni mwanamke mwenye tuache kasumba hiyo,” amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), Sharifa Suleiman amesema baraza hilo lipo tayari kuitekeleza kwa vitendo ajenda ya ‘No reform no election’ ili kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi.
Leo Jumamosi Machi 8, 2025 akitoa hotuba kwa wanawake wa Bawacha kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake (IWD), jijini Dar es Salaam amesema:
“Kina mama wa Bawacha tupo tayari kwa mapambano, tumeanza na Mungu tutamaliza na Mungu, tutaifanya ‘No reforms no election’ kwa vitendo,” amesema Sharifa.
Chadema chini ya Mwenyekiti wake, Tundu Lissu inasimamia ajenda hiyo ikilenga kuhakikisha yanakuwapo mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi nchini.
Awali, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema wakati uteuzi wa kurugenzi za chama hicho ukiendelea, alishauri kamati kuu ya chama kuwafikiria wanawake kwenye nafasi hizo.
Amesema wanawake wana nguvu kubwa ya wingi wa kushawishi mkakati wa ‘Hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi’ kwa sababu sauti zao ni kubwa.
“Hata mngekuwa wachache mna uwezo mkubwa kutokana na sauti zenu, sasa tunawaomba huo uwezo mlionao zungumzeni ‘No reform no election’ ili watawala wasikie.
“Pia mna nguvu ya ushawishi popote mtakapozungumza, mna uwezo wa uvumilivu tena wa kipekee. Sasa mapambano tunayoelekea ni magumu sana tunahitaji uvumilivu wenu wa hali ya juu,” amesema.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu katika hotuba ya siku ya IWD ametaka wakumbuke kuwa hawapiganii tu haki za wanawake bali mustakabali wa Taifa.
“Wakati ni sasa, mapambano ni yetu. Tuamke, tupinge na tusonge mbele pamoja kuelekea ushindi. Tunajua njia itakuwa ngumu. Tunajua changamoto tunazokutana nazo ni kubwa. Lakini azma yetu ni kubwa zaidi,” amesema.

Akizungumzia nafasi ya ngome ya wanawake ya chama hicho katika kudai mageuzi amesema ‘operesheni linda demokrasia’ ni nyenzo ya kudai uchaguzi huru na wenye kuaminika.
“Ni operesheni ya kupinga hila, hujuma na mifumo kandamizi ya kiuchaguzi,” amesema.
Amesema ngome ya wanawake ina jukumu la kuhakikisha wanawake wa Tanzania wanakuwa mstari wa mbele katika kudai mageuzi ya kisiasa, kuleta mabadiliko ya mfumo wa kiutawala na kupambana na dhuluma zote dhidi ya haki za wanawake na Taifa kwa ujumla.
Semu amesema hakuna Taifa lililokombolewa bila nguvu ya wanawake.
Pia amesema wanawake wanapaswa kupigania haki za msingi mijini na vijijini kuanzia huduma bora za afya bure na zinazopatikana kwa wote.
“Ni wito kwa kila mwanamke katika ACT-Wazalendo kusimama, kuongoza na kuleta mabadiliko. Hatukuja kuonyesha tu yale tunayoyapitia, tupo hapa kudai haki yetu ya kuwa sehemu ya jamii, na hatutolala mpaka tufikie malengo yetu,” amesema.