DABI ya Kariakoo ina utamu wake, ikiwamo baadhi ya wanandugu kuweka historia ya kucheza mechi hizo za Watani wa Jadi. Ndio ipo orodha ya wanandugu waliokipiga dabi lakini kila mmoja na wakati wake au kuwa katika timu moja.
Nyota Haidar Abeid ‘Muchacho’ na Khalid Abeid ni kati ya ndugu waliokipiga dabi, mastaa wa ukoo wa Njohole, kuanzia Nico Njohole, Deo Njohole hadi Renatus Njohole wameicheza dabi, kama ilivyo kwa Abuu Juma na Makumbi Juma, Idd Moshi na Haruna Moshi, Mussa Kihwelo, Jamhuri Kihwelo na Mtwa Kihwelo ni koo nyingine zilizokipiga katika Dabi.
Hata hivyo, rekodi iliwekwa mwaka 1993 na ukoo wa Mgaya kutokea pale Tanga, yaani Issa Athuman na mdogo wake, Kassongo Athuman walipovaana kila mmoja na chama lake na kukaushiana kama hawajuani ndani ya dk 90. Katika pambano hilo lililopigwa Machi 27, Issa alimtambia mdogo wake baada ya Yanga kushinda 2-1, mabao yote ya washindi yakiwekwa kimiani na Said Mwamba ‘Kizota’, huku lile la kufutia machozi la Simba ya Kassongo likiwekwa kimiani na Edward Chumila ‘Edo Boy. Hii si mchezo!