ALIYEKUWA Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro amesikitishwa na kitendo cha mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Simba uliopaswa kuchezwa leo kushindwa kuchezwa, huku akiitaka Bodi ya Ligi (TPLB), kufungiwa milele kwa kushindwa kusimamia.
Kupitia mtandao wake wa kijamii, Muro aliandika; “Mechi ya Yanga na Simba imekuwa ikitumika kama sehemu ya kilele cha burudani ya mpira nchini na katika burudani hii kama ambavyo Mheshimiwa Rais Samia amesema siku zote huambatana na furaha kuu na pia hutoa fursa lukuki kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogowadogo, leo nina hoja chache hebu tutafakari pamoja;
“Katika taarifa yao rasmi kwa vyombo vya habari ambayo nimeambatanisha hapa kama rejea, Bodi ya ligi imekiri kuwa uongozi wa Simba hawakutoa taarifa, wanakwenda kufanya mazoezi uwanja wa taifa kwa mamlaka husika kitu ambacho ni kinyume cha taratibu.
“Cha kushangaza wanaahirisha mechi kuchunguza vurugu zilizotokea getini wakati mmeshasema wahusika walikwenda bila ya taarifa, naamini pangekuwapo na taarifa pangefanyika maandalizi ya kutosha kwa wao kufanya mazoezi, ila nashangaa Bodi ya Ligi inafanyaje uchunguzi kwenye masuala ya jinai pasipo kuwa na taaluma ya jinai? Nilidhani hili jambo vingeachiwa vyombo vyenye mamlaka ya uchunguzi vifanye kazi.
“Nina hoja chache za kuuliza hivi tukio hili kweli ndio linasabanisha mechi kuahirishwa? Najiuliza Bodi ya Ligi na TFF hapakuwa hata na mtu mmoja mwenye busara na ushawishi wa kutatua hii changamoto na ngoma ikapigwa? Kama ndivyo basi wote wanakosa legitimacy (uhalali) wa kuwa viongozi wa ushawishi.”
Muro alihoji: “Kuna wapenda michezo wametoka mikoani na wametumia nauli zao, fedha za kujikimu na muda wao, hawa tunawaambia nini?
“Pia, alihoji wako wajasiriamali walikopa fedha ya kuanzisha biashara ndogondogo pale uwanjani mfano uuzaji jezi, skafu, vinywaji baridi, wako waliopika chakula mfano kuku, biriani pilau na vingine hawa tunawaambia nini?
“Wako wadhamini waliotangaza kuonyesha mechi ‘live’ watu wakalipia visimbuzi vyao, wadhamini wakalipia matangazo ya biashara leo tunawaambia nini?
“Wako watu wa Yanga uongozi uliandaa timu kwa gharama kubwa kukaa kambini maandalizi ya mechi ya leo tunawaambia nini hawa?
“Pia alihoji viongozi wa kusimamia mpira kama mechi kamishna, msimamizi wa kituo, waamuzi wametoka mikoani wamepewa posho na fedha za kujikimu na wamekaa hotelini leo tunawaambia warudishe pesa?”
Muro alihoji hasara pia za mchezo wa leo ni nani atagharamia kuzilipa, huku akidai ni ufisadi tena ufisadi wa wazi na kuwataka Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kuingilia kati jambo hili.
Katika hitimisho lake, Muro alihoji maswali manne akianza na kuuliza uzalendo uko wapi wa kusimamia sheria na kanuni? Iko wapi dhana ya FIFA Fair Play?, Ziko wapi 4R za Rais Samia? na iko wapi kodi ya TRA?
Pia aliomba wataalamu wa sheria ikiwamo chama cha wanasheria nguli nchini (TLS) wasaidie kufungua kesi katika vyombo vya kimichezo katika Mahakama ya Usuluhishi wa Kimichezo wa Kimataifa (CAS), huku akimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ushindani (FCC), William Eriyo kushughulikia jambo hilo, licha ya yeye kuwa mwanachama mwandamizi wa Simba.