Arusha/Dar. Wakati Watanzania wakisubiri kwa hamu kuanza utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote, Rais Samia Suluhu Hassan ametaja hatua iliyofikiwa katika mchakato huo, akieleza ni jambo zito.
Mchakato ulianza kufanyiwa kazi miaka kadhaa iliyopita, ugumu ukiibuka katika maeneo kadhaa, likiwamo la ukusanyaji wa fedha za kuendesha skimu kuwezesha upatikanaji wa bima kwa watu wasio na uwezo.
Akizungumza leo Machi 8, 2025 jijini Arusha wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani (IWD), Rais Samia amesema uzito wa mpango huo unasababishwa na umuhimu wake.
Amesema hayo alipozungumzia namna Serikali ilivyotekeleza malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDG) ambayo ndani yake lipo linaloelekeza kuhusu huduma bora za afya.
Samia amelishukuru Bunge kwa kupitisha mpango huo, akisema kwa sasa limebaki upande wa Serikali kulifanyia kazi, akieleza wanafanya marekebisho mara kwa mara ili uwe sawa.
“Jambo hili ni zito na si jepesi, tunalishukuru Bunge kwa kulipitisha, kwa sasa limebaki upande wetu (Serikali), tunakwenda tunajaribu halafu tunarudi kurekebisha,” amesema.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya Desemba 4, 2023 inasema muswada wa bima ya afya kwa wote ulishasainiwa na Rais na kuwa sheria kamili, baada ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Desemba mosi, 2023.
Bunge liliupitisha muswada huo Novemba 2, 2023, hatua iliyofikiwa baada ya mkwamo uliokuwepo kwa takribani miaka mitano tangu ulipofufuliwa upya mwaka 2018.
Katika kufanikisha huduma, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi iliweka msisitizo wa umuhimu wa kuwa na mfuko kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na Serikali iusimamie kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya.
Kupitia sheria hiyo kutakuwa na utaratibu wa utambuzi na usajili wa kundi la watu wasio na uwezo, kwa lengo la kuhakikisha wanapata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.
Kundi hilo litajumuishwa kwenye skimu ya Bima ya Afya ya Umma kwa namna itakavyoainishwa kwenye kanuni zitakazotungwa.
Vyanzo vya mapato ya skimu hiyo vilitajwa kuwa sehemu ya mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa, kwenye vinywaji vyenye kaboni, vinywaji vikali, bidhaa za vipodozi, kodi ya michezo ya kubahatisha, ada ya bima za vyombo vya moto na mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki.
Rais Samia akizungumza katika maadhimisho jijini Arusha, ametaja faida ya mpango huo akisema licha ya kutoa huduma kwa wananchi wengi, utaimarisha ubora wa huduma za afya.
“Tunataka kila Mtanzania awe na bima ya afya ili tuweze kudhibiti na kulinda hadhi ya huduma za afya tuliyonayo. Hivi ni vituo vya afya, hospitali kuna viwango vyao na ili tuvifikie lazima tuchangie huduma za afya. Kwa hiyo, hili litakuja, tulichukue kama Watanzania ili lifanikiwe,” amesema.
Serikali pia, imeshawasilisha bungeni Muswada wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) 2025 ukiwa na lengo la kuufanyia marekebisho ikiwamo usajili wa wanachama wa sekta binafsi, sekta isiyo rasmi na watu wasio na uwezo.
Muswada huo uliosomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa 18 wa Bunge uliomazika Februari 14, 2025, umependekeza marekebisho yatakayoruhusu usajili mpana wa wanachama zaidi ya watumishi wa umma.
Lengo la Serikali kuwasilisha muswada huo ni kuoanisha shughuli za mfuko huo na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (UHI).
Rais Samia pia, ameikumbusha jamii kuhusu ajenda ya kizazi chenye usawa akieleza harakati za usawa wa kijinsia zinapaswa kurithishwa kwa kizazi kijacho.
Amesema kwa sasa Tanzania inakabiliwa na changamoto ya maadili, hivyo ni jukumu la kila mwanajamii kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.
“Uendelevu wa harakati hizi utategemea kizazi kipya cha watoto wetu wa kike na wa kiume tunachokijenga, tuna kazi ya kujenga kizazi chetu chenye maadili na kuheshimiana na hii si kazi ya sekta moja.
“Ni kazi ya wazazi, Serikali, viongozi wa dini, walimu na jamii kwa jumla. Tuna kazi ya kurudi nyuma kulea watoto wetu. Kujenga kizazi kitakachokuwa na maadili ya Kitanzania na kizazi kitakachoheshimiana,” amesema.
Rais Samia amesema kuna umuhimu wa kujenga kizazi cha watoto wanaojiamini na wenye uwezo wa kujenga hoja.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika leo Machi 8, 2025 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Pia, amesema wajengwe vijana watakaotambua kuwa ukubwa wa hoja yake si ukali wa sauti wala maneno yake, bali ni uzito wa hoja yake, utulivu na ufasaha wakati wa kuiwasilisha hoja yenyewe.
“Kule kusema hoja kwa ukali, sauti kali na kufoka si kujenga hoja bali ni kupotosha hoja, tujenge vijana wenye uwezo wa kuwasilisha, kutetea na kuwa na ushawishi katika hoja wanazowasilisha. Tujenge vijana wanaojitambua,” amesema.
Katika eneo la uwezeshaji wananchi kiuchumi, amesema Tanzania ina programu 75 kati ya hizo 63 zipo serikalini na 12 zinaratibwa na sekta binafsi.
Amesema mifuko na programu hizo zimewezesha utoaji wa mikopo yenye thamani ya Sh3.5 trilioni na Sh1.7 trilioni sawa na asilimia 49 zilitolewa kwa wanawake katika maeneo mbalimbali Tanzania.
Awali, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema wizara imeunda kamati maalumu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Amesema kamati hiyo itakuwa inazunguka katika vijiji na mijini, nyumba kwa nyumba kuhakikisha inawafikia wananchi, hususan wanawake.
“Viongozi wa majukwaa hayo katika kila ngazi kupitia ajenda ya ‘mwanamke funguka ongea na Samia’ watapita maeneo yote ya vijijini na mijini ili kuwaeleza wanawake fursa zilizopo katika majukwaa hayo ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ili wayatumie kujikwamua kiuchumi,” amesema.
Amesema wizara imefanya makongamano saba katika mikoa mbalimbali kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake yaliyolenga kutoa elimu kwa wanawake, ikiwamo fursa za mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Akizungumza kwa niaba ya taasisi za kaimataifa katika maadhimisho hayo, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Susan Ngongi amesema nchi imepiga hatua kubwa katika kuleta usawa wa kijinsia, haki za wanawake na kuwa na mipango ya kiuchumi inawasaidia wajasiriamali wanawake.
Amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania kutetea uwekezaji zaidi kwa wanawake na wasichana, kuimarisha ulinzi wa kisheria, kupanua fursa za kiuchumi na elimu.
“Kupitia juhudi hizi tumeona maendeleo yanayoonekana, tunapowekeza kwa wanawake na wasichana jamii nzima hustawi. Tukishirikiana sote tutaimarisha haki, kudumisha utu, usawa na uwezeshaji kwa kila mwanamke,” amesema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza katika maadhimisho hayo amesema amani ya Tanzania iko mikononi mwa wanawake.
“Wanawake tunawaomba, amani ya nchi yetu iko mikononi mwenu, msichoke kutufundisha, msichoke kutukumbusha, msichoke kutukemea kila mtakapoona tunahatarisha amani ya nchi yetu.
“Jukumu la amani ya nchi yetu ni la kinamama, sisi tutaendelea kuwa wanafunzi wenu na tutaendelea kuwasikiliza bila kujali umri wetu, bila kujali madaraka na nafasi zetu,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema maadhimisho hayo yameonesha nafasi ya mwanamke katika jamii, huku huduma mbalimbali za kijamii zikitolewa.
“Katika maadhimisho haya wananchi wa Arusha na maeneo ya jirani wamenufaika na huduma mbalimbali zikiwamo za matibabu, uwezeshwaji wa kiuchumi na msaada wa kisheria,” amesema.
Saa 5:20 leo asubuhi Rais Samia aliingia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kupokewa kwa shangwe za wananchi waliohudhuria maadhimisho hao walioanza kuingia tangu saa 12:00 asubuhi.
Samia alipokea maandamano ya wanawake walioendesha vyombo mbalimbali vya moto zikiwamo pikipiki, bajaji, magari ya utalii, magari makubwa yakiwamo ya shule na jeshi. Pia, walikuwamo waendesha mitambo ya ujenzi wa barabara.
Baadhi ya waliohudhuria maadhimisho hao na wale waliokuwa kwenye mabanda ya maonyesho walivaa sare maalumu baadhi zikiwa ni vitenge vyenye picha ya Rais Samia.\
Wanawake wilayani Mufindi mkoani Iringa wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi wanapokuwa na kesi zinazohitaji kutolewa ushaidi mzuri ili wahusika wachukuliwe hatua.

Maandamano ya Wanawake kutoka Taasisi mbalimbali za umma na binafsi yakipita mbele ya Jukwaa kuu kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika leo Machi 8, 2025 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Mkuu wa Polisi wilayani humo, Anthony Gwandu amesema hayo alipotoa elimu ya masuala yanayohusu ukatili wa kijinsia kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa wanawake wa Halmashauri ya Mji Mafinga.
Amesema jamii haipaswi kufumbia macho vitendo vya uhalifu kwa sababu polisi wapo kwa ajili ya kuwahakikishia usalama wao, hivyo kila mtu ana wajibu wa kufuata sheria za nchi.
Kaimu Mkuu wa Dawati la Jinsia wilayani humo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Andrew Ndee amewasisitza wanawake kuacha kuwa na marafiki wasiofaa, badala yake waamini wanachokijua katika mfumo wa maisha.
“Kila mwanamke ameumbwa na kipaji chake, hivyo niwombe muwe na moyo wa kujifunza kila siku kutoka kwa watu wengine popote ulipo usijione kuwa wewe unaweza, hakikisha unatumia elimu kutoka kwa watu wengine ili kufanikiwa,” amesema.
Imeandikwa na Janeth Mushi, George Helahela, Elizabeth Edward, Tuzo Mapunda, Bakari Kiango na Mary Sanyiwa