SERIKALI YAKEMEA UBAGUA WATOTO WA KIKE KWENYE URITHI

Na Seif Mangwangi, Arusha

SERIKALI kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekemea tabia ya jamii katika maeneo mbalimbali nchini kuwabagua watoto wa kike kwa kutowapatia urithi wa ardhi na mali za familia jambo ambalo limekuwa likiibua migogoro mingi katika ngazi ya familia.

Hayo yameibuka katika kliniki ya msaada wa kisheria kupitia wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi inayoendelea kutolewa jijini Arusha ikiwa ni kuelekea kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duiani ambayo kitaifa inafanyika jijii Arusha.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthoni Sanga, amesema Mkoa wa Arusha umekuwa na migogoro mingi ya ardhi inayoanzia katika ngazi ya familia na mingi ya migogoro hiyo inahusiana na urithi hivyo ameitaka jamii kuachana mara moja na mila iyo potofu ili kupunguza migogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 7, 2025 Mhandishi Sanga amesema kuwa jamii inatakiwa kubadilika na kutambua kuwa watoto wote wana haki sawa bila kujali jinsia zao ili kuondokana na changamoto hiyo ambayo pia imekuwa ikisababisha ndugu kutoelewana na hata kupelekea wengine kutendeana vitendo vibaya.

“Tumebaini migogoro mikubwa miwili ya ardhi ndiyo tatizo kubwa hususani katika mkoa wa Arusha ambayo ni migogoro ya kifamilia na ya urithi migogoro ambayo imekuwa ikileta mitafaruku na mifarakano mingi hali inayopelekea ndugu kutoelewana”, amesema katibu Mhandishi Anthony Sanga.

Amesema migogoro mingi iliyofikishwa katika kliniki hiyo inayohusu familia ni pale mmoja wa wanafamilia anapokengeuka na kuuza mali ya familia bila kushirikisha wanafamilia wenzake na hivyo kupelekea kuibuka kwa migogoro baina yao.

Mhandisi Sanga amesema hata hivyo sheria haikubaliani na upande mmoja kuchukua maamuzi ya kuuza mali ya familia hivyo wataalamu wa wizara ya Ardhi wameweza kusikiliza migogoro ya aina hiyo na kuipatia ufumbuzi na iliyoshindikana imepelekwa mbele kwenye vyombo vya kisheria kwa maamuzi.

Aidha amesema baadhi ya watu wamekuwa wakifikisha migogoro ya ardhi na nyumba kwenye kliniki hiyo lakini migogoro hiyo ilihali migogoro hiyo ipo katika ngazi ya mahakama na mingine imeshatolewa hukumu na kusema kuwa wizara haitaweza kuingilia wala kubatilisha uamuzi wowote uliokwisha tolewa na mahakama.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amesema kuwa Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa iliyolemewa sana na changamoto ya migogoro ya ardhi na kushukuru wizara kwa kuweza kambi mkoani humo na wananchi wengi kusikilizwa kero zao na kupatiwa ufumbuzi.

Pia mkuu huyo wa Mkoa alimuomba Katibu Mkuu Sanga kuongeza siku za kuendelea kusikiliza changamoto za migogoro ya ardhi na nyumba mkoani hapo kwa kuwa wahitaji wa huduma hiyo bado ni wengi na baadhi wametoka katika mikoa ya jirani kama Tanga, Kilimanjaro, Dodoma, Manyara na hata Dar es salaam.

Kwa upande wao wananchi waliohudhuria kliniki hiyo wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo ambayo wamedai imekuwa mworabaini wa matatizo ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo kwa miaka mingi

Related Posts