Sakata la Simba kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho kujiandaa na mchezo dhidi ya Yanga, Jumamosi, Machi 08, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam limechukua sura mpya kufuatia uongozi wa timu hiyo kuamua timu yao isicheze mechi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Simba leo Machi 08, 2025 saa saba kasoro usiku, imefafanua kuwa uamuzi huo umechukuliwa kwa vile kanuni zimekiukwa.
“Simba Sports Club imesikitishwa na vitendo visivyo vya kiungwana dhidi ya timu yetu kuelekea Mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Yanga, Simba ikiwa timu mgeni.
“Kwa Mujibu wa Kanuni 17(45) ya Kanuni za Ligi Kuu Bara, Timu Mgeni ina haki ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mechi katika muda tarajiwa wa mchezo husika. Kwa makusudi Simba imenyimwa haki hiyo licha ya kufika uwanjani katika muda husika.
“Katika Sintofahamu hiyo, Simba iliarifiwa na Meneja wa Uwanja kuwa hana maelekezo ya kuruhusu mazoezi kufanyika bila maelekezo ya kamishna wa Mchezo. Pamoja na Kamishna wa mchezo husika kufika, Mabaunsa wa Klabu ya Yanga walivamia Msafara wa Simba huku wakiendelea na vurugu na wakizua Msafara wa simba kuingia uwanjani kufanya mazoezi.
Jitihada za Simba kupata fumbuzi wa changamoto hiyo hazikuzaa matunda kwa zaidi ya Masaa Mawili kabla ya Simba kuondoka eneo la nje ya uwanja kwa sababu za kiusalama ambazo zimerekodiwa kwa ajili ya ushahidi.

Kufuatia ukiukwaji huo wa Taratibu za Mchezo, Simba haitoshiriki Mchezo
husika na haki zote zimehifadhia. Simba inahimiza kuchukuliwa kwa
hatua stahidi dhidi ya wahusika wote wa sakata hili,” imefafanua taarifa hiyo ya Simba.
Kanuni hiyo ya 17(45) inafafanua hivi, “Timu ngeni itafanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mechi katika muda tarajiwa wa mchezo husika. Sababu zozote za kukwamisha timu mgeni kukidhi ipasavyo au kupata haki hii zitathibitishwa kwanza na Kamishna wa mchezo.”
Simba ilienda uwanjani hapo saa 1:00 usiku muda ambao mchezo huo utachezwa kwa ajili ya kufanya mazoezini, lakini ilizuiwa na wanaosemekana kuwa makomandoo wa Yanga na hivyo kulazimika kuondoka.
Tukio hilo linakumbushia mgomo uliofanywa na Yanga, Mei 08, 2025 katika mechi dhidi ya Simba uwanjani hapohapo ambapo haikucheza mechi hiyo kwa madai kuwa muda wa mchezo ulibadilishwa kinyume na kanuni.

Mechi hiyo awali ilipangwa kuchezwa saa 11:00 jioni lakini siku ya mchezo, muda ulibadilishwa na Bodi ya Ligi Kuu hadi saa 1:00 jambo ambalo Yanga walilipinga.
Mechi hiyo ilichezwa Julai 3, 2021 na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0.